Na Carlos Claudio, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) imepongezwa kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha sekta ya elimu nchini kupitia uwekezaji wa miundombinu ya elimu, huku wadau wa maendeleo, sekta binafsi na wananchi wakihimizwa kuendelea kuchangia Mfuko wa Elimu ili kuongeza ubora wa elimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Mbadala na Elimu ya Watu Wazima Zanzibar, Mashavu Ahmada Fakih, alipotembelea banda la TEA katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.
Mashavu amesema TEA imeendelea kuwa mshirika muhimu wa Serikali katika juhudi za kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki ya elimu bila kujali eneo analoishi, kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya elimu Tanzania Bara na Zanzibar.
Ameeleza kuwa mamlaka hiyo imechangia kwa kiwango kikubwa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kupitia ujenzi wa shule mpya, ukarabati wa majengo ya elimu pamoja na matengenezo ya miundombinu katika taasisi mbalimbali za elimu.
Kwa mujibu wake, mchango wa TEA unaendelea kuwa muhimu katika kipindi ambacho Serikali inatekeleza mageuzi ya sekta ya elimu kupitia mtaala mpya unaolenga kujenga umahiri, maarifa na ujuzi kwa wanafunzi ili kuwawezesha kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Amesema uwekezaji unaofanywa na TEA unazalisha matokeo chanya kwa kuwaandaa vijana wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha, kuongeza ushindani katika soko la ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
"Elimu ni haki ya kila mwananchi na ndiyo msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Kupitia elimu, wananchi hupata maarifa, ujuzi na uwezo wa kushiriki katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya uchumi," amesema Mashavu.




Post a Comment