Na Carlos Claudio, Dar es Salaam
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imewataka Watanzania kuepuka tabia ya kuchukua sheria mikononi, ikisema vitendo hivyo ni miongoni mwa sababu zinazochochea uvunjifu wa haki za binadamu nchini.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa THBUB, Ellen Rwijage alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari katika banda la tume hiyo kwenye Viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Julai 2, 2026.
Amesema wananchi wanapaswa kufuata taratibu za kisheria na kuwasilisha malalamiko yao katika mamlaka husika badala ya kujichukulia hatua, kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha madhara makubwa na ukiukwaji wa haki za wengine.
Ameeleza kuwa THBUB inaendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi, ikiwemo kupokea na kushughulikia malalamiko yanayohusu uvunjifu wa haki za binadamu pamoja na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
“Wananchi wanapofika katika ofisi zetu wanapata nafasi ya kuwasilisha malalamiko yao, kusuluhisha migogoro inayohusu haki za binadamu, kupata elimu kuhusu haki na wajibu wao, pamoja na msaada wa kisheria katika masuala ya haki za binadamu na utawala bora,” amesema.
Amesema si kila mwananchi anayefika na malalamiko huwa amevunjiwa haki, kwani wakati mwingine changamoto hutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu sheria, haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, katika mazingira hayo THBUB hutoa maelekezo sahihi kwa mwananchi ili aweze kufika kwenye taasisi au mamlaka inayohusika na kupata huduma au haki yake kwa wakati.
Amebainisha kuwa kadiri tume inavyoendelea kutoa elimu, ndivyo wananchi wanavyozidi kujitokeza kuripoti matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora katika maeneo mbalimbali nchini.
“Uvunjifu wa haki za binadamu unaweza kusababishwa na sababu nyingi, zikiwemo kutokujua sheria, ukosefu wa uelewa wa haki na wajibu, pamoja na changamoto za kijamii, kisiasa na kiuchumi,” amesema.
Amesema THBUB inaendelea kushirikiana na Serikali, taasisi zake, asasi za kiraia na wananchi kwa ujumla katika kuhakikisha haki za Watanzania zinalindwa na kutetewa.
Aidha, amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutambua kuwa haki huenda sambamba na wajibu, hivyo kila mtu anapaswa kutimiza wajibu wake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Amesema pale wananchi na viongozi wanapotimiza wajibu wao ipasavyo, malalamiko mengi yanayohusu ukiukwaji wa haki za binadamu na utawala bora yanaweza kupungua.



Post a Comment