******
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeendesha mafunzo kwa Asasi za Kiraia na watetezi wa haki za watoto ili kuimarisha uwezo wao wa kufuatilia, kuandika ripoti na kuripoti matukio ya ukiukwaji wa haki za watoto pamoja na kukuza haki hizo katika mfumo wa haki jinai nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Alhamisi Julai 23, 2026, Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, alisema watoto ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu nchini, hivyo ni msingi muhimu wa maendeleo ya familia na taifa.
Alisema uwekezaji kwa watoto ni hatua ya kujenga kizazi chenye maadili, uzalendo na uwezo wa kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia uzalishaji na ulipaji wa kodi siku zijazo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Veronica Buchumi, alisema Tanzania ina sheria mbalimbali zinazolinda haki za mtoto, lakini utekelezaji wake unapaswa kuzingatia mazingira halisi ya jamii ili sheria hizo ziwe na matokeo yaliyokusudiwa.
Alisisitiza kuwa kila mwenye jukumu la kulinda haki za watoto anatakiwa kutambua wajibu wake ili hatua sahihi zichukuliwe mara tu ukiukwaji unapobainika.
Naye mhadhiri wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Zachayo Shigongo, alisema haki za mtoto zinahusu nyanja zote za maisha, ikiwamo kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Alieleza kuwa utetezi wa haki za watoto hauwezi kufanywa na mtu mmoja au taasisi moja pekee, bali unahitaji ushirikiano wa serikali, wadau mbalimbali na taaluma tofauti.
Mafunzo hayo yamewakutanisha washiriki wapatao 100 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kuongeza ujuzi wa vitendo katika ufuatiliaji wa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu na uandishi wa nyaraka husika.
Washiriki pia wanapatiwa mafunzo kuhusu ukusanyaji, uhakiki na utunzaji salama wa ushahidi, utoaji wa taarifa kwa kuzingatia maadili na maslahi ya mtoto, pamoja na mifumo ya rufaa na uwasilishaji wa mashauri kwa mamlaka zinazohusika.
Aidha, wanatarajiwa kuongeza uelewa kuhusu mifumo ya kitaifa, kikanda na kimataifa ya ulinzi wa haki za watoto pamoja na misingi ya haki kwa watoto ndani ya mfumo wa haki jinai.
Picha mbalimbali wakati wa mafunzo kwa Asasi za Kiraia na watetezi wa haki za watoto ili kuimarisha uwezo wao wa kufuatilia, kuandika ripoti na kuripoti matukio ya ukiukwaji wa haki za watoto pamoja na kukuza haki hizo katika mfumo wa haki jinai nchini.







Post a Comment