Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imetumia Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, maarufu Sabasaba, kutoa elimu kwa wananchi na wadau wa sekta ya utalii kuhusu fursa zitakazopatikana katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya S!TE 2026 yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 23 hadi 25, 2026.
Akizungumza katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Afisa Masoko wa Tanzania Tourist Board, Abilah Amiri, alisema bodi hiyo imeanzisha dawati maalumu katika maonesho hayo kwa lengo la kuwaelekeza wananchi na wadau namna ya kujisajili kushiriki S!TE 2026.
Alisema dawati hilo pia linatumika kuwahamasisha washiriki wa sekta ya utalii kutumia maonesho hayo kama jukwaa la kuitangaza Tanzania kimataifa, kuunganisha biashara na kupata masoko mapya ya huduma na bidhaa za utalii.
Amiri alisema S!TE 2026 inatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya waoneshaji 200 wa huduma za kitalii pamoja na wanunuzi zaidi ya 280 wa bidhaa za utalii kutoka nchi 20 duniani.
Alitaja baadhi ya masoko yanayotarajiwa kushiriki kuwa ni nchi za Ulaya Mashariki na Magharibi, Marekani, China, Urusi, Korea na India.
“Maonesho haya si ya wafanyabiashara pekee, bali yameandaliwa kuwagusa Watanzania wote. Kutakuwa na bustani ya wanyama pori na shughuli mbalimbali za utalii kwa kiingilio nafuu, hivyo tunawaalika wananchi kufika na familia zao kujionea vivutio na kujifunza kuhusu sekta ya utalii,” alisema Amiri.




Post a Comment