TTCL YAENDELEA KUWEKEZA KATIKA VITENDEA KAZI, YAKABIDHI MAGARI SITA

******

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kutekeleza mkakati wake wa kuboresha mazingira ya kazi kwa kukabidhi magari sita (6) mapya yenye thamani ya Shilingi milioni 903 kwa Meneja wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, Meneja wa Network Operations and Maintenance pamoja na Meneja wa Network Planning, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa shughuli za kiutendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Makabidhiano hayo yaliyofanyika leo katika Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam, ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL mnamo Aprili 29, 2026, wakati Shirika lilipokabidhi magari kwa baadhi ya viongozi wa idara mbalimbali, ambapo aliahidi kuendelea kuwekeza katika vitendea kazi ili kuongeza tija na ufanisi wa Shirika.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi wa Ufundi wa TTCL, Mhandisi Cecil Francis, alisema ununuzi wa magari hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka 10 wa Shirika unaolenga kuimarisha mazingira ya kazi, kuboresha usimamizi wa miundombinu ya mawasiliano na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma kwa wateja nchini.

Alisema magari hayo yatasaidia timu za kiufundi kufikia maeneo mbalimbali kwa wakati, kuongeza ufanisi katika usimamizi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano pamoja na kuhakikisha huduma za TTCL zinaendelea kutolewa kwa viwango vya juu.

"Magari haya ni mali ya Shirika. Ni wajibu wa watakaoyatumia kuyatunza, kuyatumia kwa kuzingatia maadili na kuhakikisha yanadumu ili yaendelee kutoa manufaa yaliyokusudiwa," alisema Mhandisi Francis.

Baada ya kupokea magari hayo kwa niaba ya watumiaji, Meneja wa Network Operation and Maintenance (MNOM) Mhandisi Abbas Buge aliishukuru Menejimenti ya TTCL kwa kuendelea kuwekeza katika vitendea kazi vinavyowezesha utekelezaji bora wa majukumu ya kila siku.

Alisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya Menejimenti katika kuboresha mazingira ya kazi na kuwawezesha wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

"Kwa niaba ya wafanyakazi wote waliokabidhiwa magari haya, tunatoa shukrani za dhati kwa Menejimenti ya TTCL kwa kutuamini na kuendelea kuboresha vitendea kazi. Tunaahidi kuyatunza magari haya, kuyatumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha yanachangia kuongeza ufanisi wa kazi pamoja na kuboresha huduma kwa wateja wetu," alisema.

Ununuzi wa magari hayo unaendelea kuonesha dhamira ya TTCL ya kuwekeza katika rasilimali na miundombinu ya kazi ili kuongeza tija, kuimarisha utendaji wa Shirika na kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi kwa haraka, ufanisi na ubora, sambamba na kuendeleza utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka 10 wa Shirika.








 

0/Post a Comment/Comments