.....
Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.
Wananchi wamehimizwa kurejea kwenye matumizi ya vyakula vya asili vyenye virutubisho kwa lengo la kuimarisha afya, kuongeza nguvu za mwili na kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza.
Wito huo umetolewa na Sarah Moyo, mjasiriamali wa tiba lishe, wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea banda lake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Sarah alisema lishe bora ndiyo msingi wa afya njema na kwamba jamii inapaswa kurejea kwenye matumizi ya miti na matunda ya asili yenye virutubisho muhimu kwa mwili.
Alisema miongoni mwa bidhaa anazozitoa ni bidhaa zinazotokana na mlonge, ambao alisema unaweza kutumiwa na watu wa rika mbalimbali kuanzia watoto wenye umri wa miezi sita hadi wazee, kama sehemu ya lishe yenye virutubisho.
"Mwanadamu anahitaji kula virutubisho. Tunapaswa kurudi katika matumizi ya vyakula vya asili, miti na matunda. Bidhaa zetu zinasaidia kuongeza virutubisho mwilini na kuboresha afya kwa ujumla," alisema.
Alieleza kuwa kampuni yake, Ajabu Enterprises, inayopatikana Kinondoni Mkwajuni jijini Dar es Salaam, inajishughulisha na utoaji wa bidhaa za tiba lishe na mwaka huu imewasilisha bidhaa mbalimbali zinazolenga makundi tofauti ya watumiaji.
Kwa mujibu wa Sarah, bidhaa hizo zimeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya makundi mbalimbali ikiwemo wanaume, wanawake, vijana, watoto na wazee.
Alisema baadhi ya bidhaa zimekusudiwa kusaidia kuongeza virutubisho mwilini na kuboresha afya kwa ujumla, huku akiwahimiza wananchi kupata ushauri sahihi kuhusu matumizi ya bidhaa hizo kulingana na mahitaji yao.
Sarah aliwataka wananchi wanaotembelea Maonesho ya Sabasaba kufika katika banda lao ili kupata elimu kuhusu tiba lishe na matumizi ya vyakula vya asili vinavyoweza kusaidia kuboresha afya.
Aliongeza kuwa baada ya maonesho hayo, huduma na bidhaa za kampuni hiyo zitaendelea kupatikana katika ofisi zao zilizopo Kinondoni Mkwajuni, nyuma ya msikiti, ambapo wananchi wanaweza kufika kwa ushauri na huduma zaidi.
"Tunawakaribisha wananchi wote kutembelea banda letu Sabasaba kujifunza kuhusu tiba lishe na umuhimu wa lishe bora. Baada ya maonesho, tunaendelea kutoa huduma katika ofisi zetu Kinondoni Mkwajuni," alisema.


Post a Comment