WAAJIRIWA WAPYA TRA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA, KANUNI, TARATIBU NA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

*******

Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Mcha Hassan Mcha, amewataka waajiriwa wapya wa mamlaka hiyo kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Maadili ya Utumishi wa Umma katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya wa TRA yaliyofanyika Julai 20, 2026 katika Chuo cha Kodi Dar es Salaam, Naibu Kamishna Mkuu amesema Maadili, weledi na kujituma ni nguzo katika utumishi wa Umma ili kufanikisha malengo ya ukusanyaji wa mapato na kuchangia maendeleo ya taifa.

Aidha, Naibu Kamishna Mkuu Mcha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuidhinisha ajira mpya kulingana na mahitaji ya taasisi hiyo, hatua inayokwenda kuongeza nguvu kazi na kuimarisha utendaji wa mamlaka.

Amesema TRA ni mhimili muhimu wa maendeleo ya nchi kwani mapato yanayokusanywa ndiyo yanayowezesha Serikali kujenga na kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo shule, hospitali na miundombinu mingine. 

Pamoja na hayo, amewasisitiza kutumia ipasavyo mafunzo elekezi watakayopatiwa kwa kushiriki kikamilifu, kuuliza maswali na kutoa mawazo yatakayowawezesha kuongeza uelewa na kuboresha utendaji wao kazini.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TRA Bw. Moshi Kabengwe amesema amesema waajiriwa wapya 243 wanaopokelewa hii leo wanaifanya TRA iwe na jumla ya watumishi 9,020 kwa nchi nzima.

Amesema TRA ni mahala salama pa kufanyia kazi na kuwataka watumishi hao kulinda heshima waliyopewa kwa kukusanya mapato ya Serikali kwa uadilifu kwa maendeleo ya Taifa. 

Naye Mkuu wa Chuo Cha Kodi Prof. Isaya Jairo amesema chuo hicho kipo tayari kutoa mafunzo ya awali ya Kodi na Forodha kwa waajiriwa hao na kuwakaribisha chuoni hapo.








0/Post a Comment/Comments