MWANZA
Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content Compliance Forum – LCCF 2026), litakalofanyika kuanzia Julai 22 hadi 24, 2026, katika Ukumbi wa Malaika Beach Resort jijini Mwanza.
Jukwaa hilo, linaloandaliwa na Tume ya Madini, linatarajiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini, wakiwemo makampuni ya uchimbaji wa madini, watoa huduma migodini, wafanyabiashara wa madini, taasisi za Serikali, wawekezaji pamoja na wananchi wenye shauku ya kushiriki katika maendeleo ya sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Tume ya Madini, Jukwaa litatoa fursa kwa washiriki kujifunza kupitia mawasilisho ya kitaalam, midahalo, mafunzo na maonesho yatakayolenga kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika shughuli za uchumi zinazotokana na Sekta ya Madini.
Aidha, jukwaa hilo litakuwa sehemu muhimu ya kujenga ushirikiano kati ya wadau, kubadilishana uzoefu, kujadili fursa za biashara na uwekezaji, pamoja na kuimarisha utekelezaji wa sera na kanuni za ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta hiyo.
Shughuli za jukwaa zitaanza saa 2:00 kamili asubuhi kila siku kwa muda wa siku tatu.
Tume ya Madini imewahimiza wadau wote kujisajili mapema ili kushiriki katika jukwaa hilo kupitia tovuti ya lcforum.tumemadini.go.tz, au kupata maelezo zaidi kupitia barua pepe localcontent@tumemadini.go.tz na simu +255 763 714 026.
Jukwaa la LCCF limeendelea kuwa moja ya majukwaa muhimu nchini yanayolenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa Sekta ya Madini na kuchochea ukuaji wa biashara na uwekezaji nchini.

Post a Comment