![]() |
_Aongoza zoezi la upandaji wa miti TAFORI_
_Ahimiza kukamilishwa kwa maabara ya kisasa ya utafiti
Morogoro, Julai 7, 2026. Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kwa mchango wake katika kufanya tafiti zinazochochea maendeleo ya sekta ya misitu na ufugaji nyuki nchini, huku akiitaka Taasisi hiyo kutumia fursa za biashara ya kaboni kama chanzo kipya cha mapato kwa Taasisi na Taifa kwa ujumla.
Waziri Dkt. Kijaji (Mb) ametoa kauli hiyo leo Julai 07, 2026 wakati wa ziara yake katika Makao Makuu ya TAFORI, Morogoro, ambapo alipokea taarifa ya tafiti zinazotekelezwa na Taasisi pamoja na mwelekeo wake wa baadaye. Haya yamefanyika wakati wa Kikao chake na Menejimenti ya Taasisi. Aidha, ziara hiyo pia ilihusisha zoezi la upandaji wa miti ya asili adimu ambayo Taasisi imekuwa ikifanyia utafiti.
Katika ziara hiyo, Waziri aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Bw. Daniel Charles Pancras, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Bw. Benard Marcelline, pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Bw. Emmanuel Buholelwa.
Viongozi hao walipanda miti ya Mvule (Milicia excelsa), Mkongo (Afzelia quanzensis) na Mkurungu (Pterocarpus tinctorius) katika eneo la Makao Makuu ya TAFORI kama sehemu ya kuhamasisha uhifadhi wa spishi muhimu za miti ya asili nchini.
Akizungumza na Menejimenti ya TAFORI, Waziri Dkt. Kijaji (Mb) alisema wakati umefika kwa Taasisi kuangalia kwa karibu namna ya kujiunga kikamilifu katika fursa za biashara ya kaboni kwenye majaribio ya utafiti.
"Taasisi iangalie namna ya kunufaika na biashara ya kaboni. Hii ni fursa muhimu ya kuongeza mapato ya Taasisi na Serikali kwa ujumla," alisema Waziri Kijaji (Mb).
Aidha, Waziri alisisitiza umuhimu wa kuharakisha uboreshaji wa miundombinu ya maabara za utafiti kwa kuhakikisha zinakamilika na kuwa na vifaa vya kisasa vitakavyowezesha tafiti za kisayansi katika Sekta ya Misitu na Ufugaji Nyuki kufanyika kwa viwango vya kimataifa.
"Tutafute fedha maabara hiyo ikamilike kwa wakati. Tuangalie namna maabara yetu ikamilike, ili shughuli zote muhimu za kisayansi zifanyike hapa nchini. Wataalamu tunao," alisisitiza.
Awali, akitoa taarifa ya Taasisi, Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Revocatus Mushumbusi, aliwasilisha mafanikio na changamoto katika tafiti mbalimbali zinazotekelezwa, ambazo zimekuwa na lengo la kuendeleza Sekta ya Misitu na Ufugaji Nyuki.
Aidha, Mhe. Waziri aliwataka Watumishi wa TAFORI kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, na uwajibikaji ili tafiti zinazofanywa na Taasisi ziendelee kutoa suluhisho kwa changamoto za Sekta ya Misitu na Ufugaji Nyuki na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.



Post a Comment