Na Carlos Claudio, Dar es Salaam
Wizara ya Katiba na Sheria imefanikiwa kutatua mgogoro wa malipo kati ya kampuni ya Colmat General Supplier na mkandarasi mdogo (sub-contractor), hatua iliyowezesha pande zote kufikia makubaliano ya amani bila kulazimika kupeleka shauri mahakamani.
Makubaliano hayo yalifikiwa wakati wa utoaji wa huduma za msaada wa kisheria katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kufikiwa kwa makubaliano hayo, Mkurugenzi wa Colmat General Supplier Tanziru Mahamudu Mkakere amesema ameridhishwa na namna Wizara ya Katiba na Sheria ilivyoshughulikia mgogoro huo kwa kuwapa nafasi ya kusikilizwa na kufikia suluhisho lililoridhisha pande zote.
Ameeleza kuwa mgogoro huo ulitokana na kazi ya upakaji rangi wa magari takribani 200 aliyompa mkandarasi mdogo, ambapo walikubaliana kulipana Sh. 270,000 kwa kila gari, na kufanya jumla ya malipo kufikia Sh. milioni 54.
Amesema kampuni yake ilikuwa tayari imelipa zaidi ya Sh. milioni 48, huku kiasi cha Sh. milioni sita kikisalia kutokana na changamoto za kifedha zilizochelewesha kukamilisha malipo hayo, jambo lililosababisha mkandarasi huyo kuwasilisha malalamiko yake kwa vyombo vya sheria.
"Tumefika hapa na tumepokelewa vizuri. Tumeeleza changamoto zetu, tukazungumza kwa pamoja na hatimaye tumefikia makubaliano. Tunashukuru Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kwa kutusaidia kumaliza mgogoro huu kwa njia ya maelewano," alisema.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, kampuni italipa deni lililosalia la Sh. milioni sita kwa awamu nne za Sh. milioni 1.5 kila mwisho wa mwezi, hivyo deni lote linatarajiwa kumalizika ndani ya miezi minne.
Kwa upande wake mkandarasi , Sahewa Mwamba Chando, alisema aliamua kufika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria kutafuta msaada wa kisheria baada ya malipo yake kuchelewa kwa muda mrefu.
Alisema alipokelewa vizuri na kupata usuluhishi uliowezesha pande zote kufikia makubaliano yenye manufaa kwa kila upande bila kuendelea na hatua za kufungua shauri mahakamani.
"Tumeridhika na huduma tuliyoipata. Tumefikia makubaliano ambayo hakuna upande ulioonewa, na tumesaini makubaliano rasmi ya namna malipo yatakavyofanyika. Hii imetupa suluhisho la haraka na la amani," alisema.






Post a Comment