Na Ester Maile
Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imewahimiza Watanzania kujenga utamaduni wa kutumia njia mbadala za utatuzi wa migogoro badala ya kukimbilia mahakamani, ikieleza kuwa mfumo huo husaidia pande zote zinazohusika kupata suluhu ya amani na kudumisha mshikamano wa jamii.
Hayo yalisemwa Julai 1, 2026 na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainabu Katimba, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria kwenye Viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) jijini Dar es Salaam.
Katimba alisema wizara hiyo imejitokeza katika maonesho hayo kwa lengo la kuwafikia wananchi moja kwa moja kwa kuwapatia huduma mbalimbali za kisheria pamoja na ushauri kuhusu changamoto wanazokutana nazo katika maisha yao ya kila siku.
"Nitumie fursa hii kuwakaribisha Watanzania wote kutembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria ili kupata huduma za kisheria, ushauri pamoja na elimu kuhusu haki na wajibu wao," alisema.
Alisisitiza kuwa pamoja na mahakama kuwa na mamlaka ya kusimamia utoaji wa haki, njia mbadala za utatuzi wa migogoro zina nafasi muhimu katika kujenga maridhiano na kupunguza migogoro inayoweza kudumu kwa muda mrefu.
Katimba alisema kupitia maonesho hayo, maafisa wa wizara wanazungumza na wananchi wanaofika bandarini hapo ili kuwasaidia kutambua njia sahihi za kushughulikia migogoro yao kwa mujibu wa sheria.
Aidha, alisema ametembelea banda la Tume ya Kurekebisha Sheria na kueleza kuwa taasisi hiyo ina jukumu kubwa la kufanya mapitio ya sheria mbalimbali ili ziendane na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia yanayoendelea nchini, hususan katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Alibainisha kuwa serikali inalenga kuhakikisha sheria zinakuwa wezeshi na zinakwenda sambamba na matumizi ya teknolojia ya kisasa pamoja na mifumo ya kidijitali inayoongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Katika ziara yake, Katimba pia alitembelea banda la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ambapo aliwataka maafisa wa tume hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu haki za binadamu sambamba na kuwafundisha wajibu wao kwa mujibu wa Katiba.
"Haki za kila Mtanzania zinaishia pale zinapoanza haki za wengine. Ni muhimu wananchi wakatambua kuwa pamoja na kudai haki zao, wana wajibu wa kuilinda nchi na kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Ibara ya 27 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," alisema.
Naibu Waziri huyo pia alitembelea banda la Shule ya Sheria kwa Vitendo, ambapo alipokea maelezo kuhusu mfumo mpya wa kujifunza kwa njia ya kielektroniki unaolenga kuwasaidia wanafunzi kujiandaa vizuri na mitihani pamoja na kuongeza ubora wa mafunzo ya sheria nchini.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuzalisha wanasheria wenye uwezo mkubwa wa kutoa huduma bora kwa jamii.
Katika banda la Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Katimba alisema ameridhishwa na maboresho ya utoaji wa huduma, akieleza kuwa wananchi sasa wanapata vyeti vya kuzaliwa kwa muda mfupi kutokana na kuimarishwa kwa mifumo ya kidijitali.
Aliwataka Watanzania kutumia fursa ya maonesho hayo kufika mapema katika mabanda ya taasisi mbalimbali za wizara ili kupata huduma na ushauri wa kisheria badala ya kusubiri siku za mwisho wa maonesho.
Katimba aliongeza kuwa kupitia Maonesho ya Sabasaba, Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kutekeleza kampeni ya Mama Samia Legal Aid, inayolenga kusogeza huduma za msaada wa kisheria karibu na wananchi.
Alisema wananchi wenye changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ya ardhi, familia, mirathi, talaka na masuala mengine ya kisheria wanakaribishwa kutembelea banda la wizara ili kupata ushauri na huduma bila usumbufu.
Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za haki na sheria ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki kwa wakati na kwa ufanisi.




Post a Comment