.................
Na Carlos Claudio, Dodoma
WAKALA wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) umetangaza kuongeza wigo wa mafunzo kwa viongozi wa sekta ya elimu nchini, hatua inayolenga kuimarisha uongozi, usimamizi wa shule na kuongeza ubora wa elimu unaotolewa kwa wanafunzi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 6, 2026, jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid Maulid, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa taasisi hiyo wa kuwajengea uwezo viongozi wa elimu ili waweze kukabiliana na mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya elimu na kusimamia taasisi wanazoongoza kwa ufanisi zaidi.
Amesema ADEM imeendelea kutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi kwa wakuu wa shule, walimu wakuu, maafisa elimu wa kata, halmashauri na mikoa, wathibiti ubora wa shule pamoja na viongozi wengine wa elimu, kwa lengo la kuongeza uwajibikaji na kuboresha usimamizi wa taasisi za elimu nchini.
Kwa mujibu wa Dkt. Maulid, kupitia programu ya Stashahada ya Uongozi, Usimamizi na Utawala katika Elimu (DELMA), jumla ya wahitimu 8,599 wamehitimu kati ya mwaka 2002 hadi 2025. Aidha, wahitimu 2,263 wamekamilisha Stashahada ya Uthibiti Ubora wa Shule (DSQA) kuanzia mwaka 2016 hadi 2025.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa masomo 2025/2026, ADEM ilidahili wanafunzi 2,016, wakiwemo 1,634 wa programu ya DELMA na 382 wa DSQA.
Dkt. Maulid amesema mafunzo hayo yamechangia kuimarika kwa utawala bora katika shule, usimamizi wa rasilimali za elimu, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika uongozi wa shule, pamoja na kuongeza uwajibikaji wa viongozi wa elimu.
Katika hatua nyingine, amesema ADEM inaendelea kutekeleza Mradi wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji kwa Shule za Awali na Msingi (BOOST), uliopatiwa zaidi ya Shilingi bilioni 16 kwa kipindi cha miaka mitano kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa viongozi wa elimu nchini.
Kupitia mradi huo, zaidi ya walimu wakuu 17,817, waratibu elimu kata zaidi ya 3,900, pamoja na maafisa elimu wa wilaya na mikoa wamepatiwa mafunzo ya uongozi na usimamizi wa elimu kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma katika shule za umma.
"Mbali na mafunzo, ADEM imeendelea kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu unaosaidia maboresho ya sera na mifumo ya elimu. Pia imepanua ushirikiano na taasisi mbalimbali za ndani na kimataifa ili kuimarisha ubora wa mafunzo na matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu," amesema Dkt. Maulid.
Amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, ADEM inalenga kuongeza udahili wa wanafunzi wa mafunzo ya muda mrefu kutoka 2,016 hadi 3,500, sambamba na kuanzisha programu mpya za mafunzo, kupanua matumizi ya TEHAMA na kuboresha miundombinu ya kampasi zake za Bagamoyo, Mbeya na Mwanza.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa mipango hiyo unalenga kuzalisha viongozi wa elimu wenye uwezo wa kusimamia mageuzi ya sekta ya elimu na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Post a Comment