BALOZI SAID OTHMAN ATOA WITO KWA SERIKALI KUONGEZA UFADHILI WA HIFADHI YA MICHORO YA MIAMBA KONDOA

.....


Na Carlos Claudio, Kondoa

Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Said Othman Yakubu, ameiomba Serikali kuongeza rasilimali fedha kwa ajili ya uhifadhi na uendelezaji wa eneo la michoro ya miamba ya Kondoa.

Balozi Said ametoa wito huo wakati wa ziara yake katika eneo hilo, ambapo amesema uwekezaji zaidi katika uhifadhi wa eneo hilo ni muhimu kutokana na mchango wake katika kuitangaza Tanzania kimataifa, kuvutia watalii na kuongeza mapato ya Serikali, hususan fedha za kigeni.

Amesema Tanzania kwa sasa ni mjumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO, huku ikiwa pia Mwenyekiti wa Kundi la Afrika, hivyo ziara yake imelenga kujionea kwa vitendo namna maeneo ya urithi wa dunia nchini yanavyohifadhiwa na kuendeshwa.

“Ni kuendelea kutoa wito kwa viongozi wetu serikalini kuliangalia kwa jicho la ufadhili eneo hili, waweze kuongeza rasilimali fedha kwa sababu ni eneo linatambuliwa kwa urithi wa dunia,” amesema Balozi Said.

Amesema uhifadhi wa michoro hiyo una umuhimu mkubwa kwa sekta ya utalii, akieleza kuwa endapo eneo hilo litashindwa kuhifadhiwa ipasavyo na kupoteza hadhi yake, idadi ya watalii inaweza kupungua na hivyo kuathiri mapato ya Serikali.

Balozi Said ameeleza kuwa baadhi ya changamoto zinazohitaji rasilimali zaidi ni pamoja na vumbi linalofifisha michoro ya miamba, vyanzo vya maji vinavyoweza kuharibu michoro hiyo pamoja na miundombinu inayohitajika kwa ajili ya kuhifadhi na kurahisisha upatikanaji wa eneo hilo.

Amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali kupitia Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), pamoja na uongozi wa kituo hicho, katika kuboresha mazingira ya eneo hilo.

Kwa mujibu wa Balozi Said, tangu eneo hilo lilipohamishiwa chini ya TFS, hatua mbalimbali zimechukuliwa, ikiwemo uboreshaji wa njia zinazowawezesha wageni kufika katika maeneo ya michoro hiyo kwa urahisi katika majira mbalimbali ya mwaka.

Aidha, amesema UNESCO imekuwa ikitoa msaada wa kifedha katika juhudi za uhifadhi, ikiwemo kusaidia kukabiliana na changamoto ya vumbi linaloweza kuathiri michoro ya kale.

Balozi Said ameitaka pia TFS na uongozi wa kituo hicho kutumia fursa za ufadhili zinazotolewa na UNESCO, akieleza kuwa kwa sasa dirisha la ufadhili kwa maeneo ya urithi wa dunia limetangazwa.

Amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na wahusika kuhakikisha maombi ya ufadhili yanaandaliwa kwa kuzingatia vigezo vinavyohitajika, ili kuongeza uwezekano wa kupata fedha za kukabiliana na changamoto zinazolikabili eneo hilo.

Ziara hiyo pia imelenga Balozi huyo kujionea mwenyewe hali ya uhifadhi wa maeneo yanayotambuliwa na UNESCO nchini, ili aweze kupata uelewa wa moja kwa moja utakaomsaidia kuyaelezea na kuyatetea katika majukwaa ya kimataifa.

Balozi Said amewashukuru Mkuu wa Kituo, Bwana Zuberi, pamoja na timu yake na uongozi wa TFS kwa mapokezi na juhudi wanazofanya katika kulinda urithi huo wa kihistoria.






 

0/Post a Comment/Comments