BIHARAMULO.
"ROHO ya halmashauri ni Mapato" ndivyo wasemavyo waungwana, huku pongezi nyingi zikielekezwa kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo, kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa aslimia 14.
Hatua hiyo ni mwendelezo wa mafanikio baada ya mwaka 2024/25 kukusanya mapato ya ndani kiasi cha shilingi Bilioni 3,950,983,410.16 ukilinganisha na kiasi cha Bilioni 4,815,019,091.77 kwa mwaka 2025/26.
Pongezi nyingi zimeelekezwa kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Innocent Mkandara, kwa kuimarisha ukusanyaji na usimamizi thabiti wa fedha za umma.
Wakiwa kwenye kikao cha kufunga mwaka wa fedha 2025/26 madiwani hao pia wameshauri bajeti ijayo ijikite kwenye ukamilishaji wa miradi kipolo ambayo baadhi yake ina zaidi ya miaka 20 pasipo kukamilika.
"Pamoja na mafanikio makubwa ya kuvuka lengo la ukusanyaji mapato ya ndani, nishauri bajeti ijayo ya 2026/27 ijikite kwenye kutatua changamoto za maboma ya zahanati, shule na vituo vya afya ambayo mengine yana miaka 20 pasipo kukamilika licha ya kutumia fedha nyingi za Umma" amesema Aniceth Bruno, Diwani wa Kata ya Runazi.
Kwa mujibu wa utekelezaji wa bajeti kuanzia Julai 2, 2025 hadi Juni 30, 2026 halmashauri hiyo ilipokea kiasi cha Tsh. Bilioni 53,461,132,163.52 ya lengo la Bilioni 51,057,191,000, ambayo ni sawa na aslimia 101.
Vilevile wamewashauri watumishi wa halmashauri hiyo kuendeleza uhusiano mwema na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuendelea kukusanya mapato ya ndani kwa ufanisi zaidi kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Apolinary Mugarula, ametumia fursa hiyo kuwasisitiza madiwani kusimamia vyema utekelezaji wa fedha za miradi katika Kata zao pamoja na kuhamasisha jamii kuendelea kulipa kodi na tozo mbalimbali zilizoainishwa kisheria.



Post a Comment