FDH YAWATAKA WATU WENYE ULEMAVU KUPIMA AFYA ZAO MARA KWA MARA YAIPONGEZA TACAIDS KWA UJUMUISHAJI


..................

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Shirika la Foundation for Disabilities Hope (FDH) limeipongeza Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa juhudi zake za kuhakikisha watu wenye ulemavu wanajumuishwa kikamilifu katika programu na mikakati ya mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa FDH, Maiko Salali, amesema ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika mapambano dhidi ya UKIMWI ni muhimu kwa kuwa kundi hilo ni sehemu ya jamii na linahitaji kupata elimu, taarifa na huduma za afya zinazozingatia mahitaji yao.

Amesema TACAIDS imekuwa ikishirikisha watu wenye ulemavu katika programu mbalimbali za kuongeza uelewa kuhusu VVU na UKIMWI, hatua ambayo imewawezesha kushiriki kikamilifu katika juhudi za kitaifa za kudhibiti maambukizi.

“Tunapongeza sana TACAIDS kwa namna ambavyo imekuwa ikiwajumuisha watu wenye ulemavu katika mapambano dhidi ya UKIMWI. Tume imekuwa ikiweka mikakati ya kuhakikisha hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma,” amesema Salali.

Salali amesema pamoja na juhudi hizo, TACAIDS imeendelea kuweka na kuboresha mazingira na miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu, ili kuwawezesha kupata elimu na taarifa sahihi kuhusu VVU pamoja na kushiriki katika programu mbalimbali za afya.

Amesema FDH inaamini kuwa ujumuishaji wa watu wenye ulemavu ni sehemu muhimu ya kufikia malengo ya kitaifa ya kutokomeza UKIMWI, kwa kuwa mafanikio katika mapambano hayo yanahitaji ushiriki wa kila kundi katika jamii.

Aidha, amewataka watu wenye ulemavu nchini kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara, kupata taarifa sahihi kuhusu VVU na kushiriki kikamilifu katika programu zinazolenga kudhibiti maambukizi.

Kwa upande wake, amesema FDH imepanga kuendesha kampeni maalumu ya “NA SISI TUPO” itakayolenga kutoa elimu kwa jamii, hususan watu wenye ulemavu na vijana, kuhusu umuhimu wa kupima afya, kujikinga na VVU na kuchukua hatua stahiki za kulinda afya zao.

Salali amesema kampeni hiyo inalenga kuwafikia watu wenye ulemavu wengi zaidi na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya UKIMWI, akisisitiza kuwa Tanzania salama dhidi ya UKIMWI itajengwa kwa ushiriki wa kila Mtanzania bila kujali hali yake.
 

0/Post a Comment/Comments