....
Na Carlos Claudio, Dodoma
Mwanamuziki mkongwe nchini, Khalid Mohamed maarufu TID, ameipongeza Aven Pro Live Recording Studios ya jijini Dodoma kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika vifaa vya kisasa vya kurekodia muziki, akisema studio hiyo imejengwa kwa viwango vya juu na inaweza kuwa kituo muhimu kwa muziki wa live band nchini.
TID aliyasema hayo jijini Dodoma baada ya kutembelea na kukagua studio hiyo, ambapo amesema amevutiwa zaidi na vifaa vilivyowekwa kwa ajili ya kurekodi wanamuziki na waimbaji kwa wakati mmoja.
“Nilipofika hapa, baada ya kuangalia equipment nilishtuka. Nikasema hii investment haijakwenda hivi.
This is a state-of-the-art live band equipment,” amesema TID.
Amesema kurekodi muziki wa live band ni kazi inayohitaji vifaa na mazingira maalumu kwa kuwa kila mwanamuziki huhitaji kurekodiwa katika channel yake, jambo ambalo kwa muda mrefu limekuwa changamoto kwa wasanii wanaofanya muziki huo, hususan jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa TID, uwepo wa Aven Pro Live Recording Studios unaweza kupunguza changamoto hiyo kwa wasanii, bendi na vikundi vya waimbaji, kwa kuwa studio hiyo ina uwezo wa kuwakutanisha wanamuziki wengi na kurekodi kazi zao kwa wakati mmoja.
“Kurekodi live ni changamoto kwa kutanisha wanamuziki wote, kila mmoja yuko kwenye channel yake. Kwa hiyo hili la kusema unarekodi watu wote kwa wakati mmoja ni jambo zito sana kwa wasanii wa Dodoma, na si Dodoma tu bali Tanzania nzima,” amesema.
Aidha, TID ametoa ofa maalumu kwa msanii mmoja wa Dodoma ambaye atakuwa tayari kutumia fursa hiyo, akisema yeye pamoja na Heroes Band watamsaidia msanii huyo kurekodi wimbo wa live band pamoja na kutengenezewa video ya kurekodiwa moja kwa moja (live recording video).
“Nataka nitoe offer ya kurekodi wimbo mmoja wa live band kwa msanii wa Dodoma ambaye anatuangalia hapa. Aje hapa, tumuangalie, tumpe nafasi ya kurekodi na wao. Tena hiyo itakuwa ni visual pia na live recording,” amesema.
Amesema hatua hiyo inalenga kuwapa nafasi wasanii chipukizi wa Dodoma kuonesha vipaji vyao na kutumia miundombinu iliyopo katika studio hiyo, huku akiwataka wasanii wengine kuchangamkia fursa hiyo.
TID, ambaye amesema amekuwa akiishi na kufanya shughuli zake za muziki jijini Dodoma kwa takribani miaka minne, amesema uwekezaji huo ni hatua muhimu kwa maendeleo ya muziki wa live band na umeonesha kuwa wanamuziki wa aina hiyo nao wanaweza kupata mazingira bora ya kufanya kazi bila kulazimika kusafiri kwenda miji mingine.
Kwa upande wake, uongozi wa Aven Pro Live Recording Studios umesema studio hiyo imewekeza katika vifaa vya kisasa na vya ubora wa juu kwa ajili ya kutoa huduma za kurekodi muziki, hususan live band, huku ikiwa na nafasi inayoweza kuhudumia zaidi ya watu 50 kwa wakati mmoja.
“Studio yetu ina equipment ambazo ziko very modern. Lakini pia studio yetu ina ukubwa ambao inaweza kubeba more than 50 people wakiwa na record ama kufanya shughuli zote ambazo zinafanyika kwenye studio,” amesema uongozi wa studio hiyo.
Studio hiyo pia inalenga kuwa kituo cha mafunzo kwa vijana wanaotaka kujifunza upigaji wa vyombo mbalimbali vya muziki, ikiwemo drums, keyboards na vyombo vingine, pamoja na kuwajengea uwezo waimbaji kupitia mafunzo maalumu ya sauti
TID amesema fursa hiyo haijaishia kwa wasanii pekee, bali pia vikundi vya kwaya na bendi kutoka maeneo mbalimbali nchini, akivitaka kutumia studio hiyo kama sehemu ya kurekodia na kuandaa kazi zao za muziki.
“Watu wa choir, this is your home, this is your destination. Watu wa live band Tanzania nzima, this is your destination,” amesema.
Amesema yeye pamoja na Heroes Band watakuwa wakifanya sessions katika studio hiyo ili kutoa mfano wa namna vifaa na mazingira ya studio hiyo vinavyoweza kutumika katika kurekodi muziki wa moja kwa moja.
Aven Pro Live Recording Studios imetangaza kuwa uzinduzi rasmi wa studio hiyo utafanyika Septemba 18, 2026, ambapo kutafanyika tukio maalumu la uzinduzi litakalowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya muziki


Post a Comment