Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kushiriki Maonesho ya 32 ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane, ukiwahimiza wafanyabiashara, wakulima na wajasiriamali kutumia fursa hiyo kurasimisha shughuli zao za kiuchumi na kupata huduma mbalimbali za usajili kwa urahisi.
Huduma hizo zinatolewa katika Viwanja vya Nane Nane Nzuguni, Dodoma kuanzia Agosti 1 hadi 8, 2026, ambapo wananchi wanapata huduma zote muhimu zinazotolewa na BRELA bila kulazimika kufika katika ofisi za taasisi hiyo.
Akizungumza katika Maonyesho ya Kitaifa ya Wakulima 'Nane Nane, Afisa Usajili wa BRELA, Yusuf Mwasakafyuka, amesema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa haraka huku wakipatiwa elimu kuhusu umuhimu wa kurasimisha biashara zao ili ziweze kukua na kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi.
Amesema huduma zinazotolewa ni pamoja na usajili wa majina ya biashara, usajili wa kampuni, utoaji wa Leseni za Biashara Kundi A, usajili wa alama za biashara na viwanda pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu huduma zote zinazotolewa na BRELA.
"Tunawakaribisha wafanyabiashara, wakulima na wananchi wote wanaofanya shughuli za kiuchumi kutembelea banda letu. Hapa wanapata huduma zote ambazo kwa kawaida hupatikana katika ofisi zetu pamoja na elimu itakayowasaidia kurasimisha biashara zao na kuzifanya zikue zaidi," amesema.
Amefafanua kuwa maonesho hayo pia yanatumika kuutambulisha mfumo mpya wa usajili ulioboreshwa, ambao umeongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa njia ya kidijitali na kurahisisha hatua mbalimbali za usajili.
Kwa mujibu wake, kupitia mfumo huo mpya, wananchi wanaweza kufanya maombi ya huduma, kuwasilisha nyaraka mbalimbali na kufuatilia maendeleo ya maombi yao kwa njia ya mtandao bila kufika ofisini, hatua inayookoa muda na gharama.
"Lengo la maboresho haya ni kuhakikisha huduma zinapatikana kwa urahisi zaidi. Leo hii mteja anaweza kuwasilisha nyaraka akiwa nyumbani, ofisini au mahali popote alipo bila kulazimika kusafiri kuja BRELA," amesema.
Mwasakafyuka amesema mfumo huo pia umeongeza uwazi katika upatikanaji wa taarifa za kampuni na kuimarisha usalama wa taarifa za wanahisa, ambapo wahusika hupata taarifa kila kampuni inapofanya mabadiliko yanayohusu umiliki au taarifa nyingine muhimu.
Ameongeza kuwa ili kutumia mfumo huo kwa ufanisi, mwananchi anatakiwa kuwa na Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA), namba ya simu inayotumika na anuani sahihi ya barua pepe, ambazo ni muhimu katika usajili na matumizi ya huduma za kidijitali.
Aidha, amewahimiza wakulima na wajasiriamali wanaoshiriki Maonesho ya Nane Nane kutumia nafasi hiyo kurasimisha biashara zao, akieleza kuwa urasimishaji unafungua fursa za kupata mikopo, masoko mapana, zabuni na kushirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha na maendeleo.
BRELA ni taasisi inayosimamia usajili na urasimishaji wa biashara nchini, ikiwemo usajili wa kampuni, majina ya biashara, alama za biashara, pamoja na utoaji wa Leseni za Biashara Kundi A.
Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Nane Nane, taasisi hiyo inalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuendelea kuhamasisha ukuaji wa biashara rasmi kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Maonyesho ya Kitaifa ya Wakulima 'Nane Nane' Kwa mwaka huu 2026 yanaongozwa na kauli mbiu isemayo "Tambua soko,ongeza Toka kutekeleza Dira 2050".

Post a Comment