NA: MWANDISHI WETU
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Mary Chatanda, ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Songwe kwa kufanikisha miradi mingi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi.
Chatanda ametoa pongezi hizo, Agosti 3, wilayani Songwe, katika ziara maalum ya viongozi wa UWT Taifa kukagua shughuli mbalimbali mkoani Songwe.
Amesema kuwa, serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imejikita katika kutatua kero za wananchi kupitia miradi ya maendeleo.
"Nimejionea kwa macho kazi nzuri zimefanyika Songwe, mmegusa maisha ya wananchi, fedha za mikopo ya asilimia kumi zinafika kwa vijana, wanawake na wenye mahitaji maalum, hakika Songwe mmeonyesha mfano mzuri wa kuigwa," amesema Chatanda.
Akiwa Songwe, Chatanda na wajumbe wa Jumuiya hiyo, walipata fursa ya kutembelea kikundi cha wanawake cha 'Mama ni Nguzo' kinachojishughulisha na uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya dhahabu. Kikundi hiki kimenufaika na mkopo wa shilingi milioni 100.
Aidha, walitembelea kikundi cha waponda kokoto Saza ambacho kimeonyesha uaminifu wa kurejesha mkopo wote wa shilingi milioni 23 waliokopeshwa awali huku uongozi wa Halmashauri ukijipanga kuwakopesha gari aina ya fuso ili kubeba mawe na hatimaye waweze kukuza mradi wao.
Katika hatua nyingine, wajumbe hao walitembelea mradi wa ujenzi wa Soko la Madini la CPA. Cecilia Kavishe, ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 99.
Sanjari na hilo, wametembelea mradi wa ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UWT wilaya, huku wakipongeza hatua nzuri iliyofikiwa.
Ziara hiyo ya siku tatu mkoani humo ni mahsusi kwa ajili ya kukagua uhai wa Chama, Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025-2030.
Vilevile, kufanya mikutano ya ndani, kuongea na wanachama na wananchi kuwapongeza kwa kuendelea kuwa na imani na Chama hicho katika kuwatumikia.







Post a Comment