CP MKAMA APONGEZA USHIRIKIANO OFISI YA RC MWANZA, VYOMBO VYA USALAMA


 *****

Kamishna wa Polisi Jamii, CP Alex Mkama leo Agosti 4, 2026 ametembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambapo amepokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Amir Mkalipa aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa.

Akimkaribisha, Mhe. Mkalipa amesema Mkoa wa Mwanza unaendelea kuwa salama na wenye utulivu hali inayowapa wananchi fursa ya kuendelea na shughuli zao za kijamii na kiuchumi bila hofu huku akidokeza kuwa mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi, vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi.

m

Mhe. Mkalipa amemkaribisha CP Mkama Mkoani Mwanza na kumueleza kuwa mkoa uko tayari kuendelea kupokea ushauri, maelekezo na miongozo kutoka Makao Makuu ya Polisi ili kuimarisha zaidi utekelezaji wa falsafa ya Polisi Jamii na kudumisha amani na usalama.

CP Mkama amesema lengo la ziara hiyo ni kukutana na kufanya mazungumzo kuhusu utekelezaji wa shughuli za Polisi Jamii mkoani Mwanza, ikiwemo kutathmini hatua zilizofikiwa, kuangalia mafanikio yaliyopatikana na kubaini maeneo yanayohitaji kuboreshwa ili kuongeza ufanisi katika ushirikishwaji wa wananchi kwenye masuala ya usalama.

Pia amesema amekuja kujionea shughuli mbalimbali za Polisi Jamii zinazotekelezwa mkoani humo, pamoja na kupata tathmini ya namna zinavyoendeshwa ili kuendelea kuziimarisha.

Katika hatua nyingine, CP Mkama amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa ushirikiano na miongozo ambayo amekuwa akiitoa kwa Jeshi la Polisi katika vipindi mbalimbali. Amesema Mkuu wa Mkoa amekuwa mstari wa mbele kutoa ushauri na maelekezo yanayochangia kuimarisha utendaji wa Jeshi la Polisi na usalama wa wananchi.

Aidha, ameupongeza ushirikiano uliopo kati ya Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama mkoani Mwanza, akieleza kuwa ushirikiano huo ndio msingi halisi wa dhana ya Polisi Jamii.

"Ushirikiano huu unaooneshwa na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi ndiyo tafsiri halisi ya Polisi Jamii, kwani usalama ni jukumu la kila mmoja," amesema CP Mkama.






0/Post a Comment/Comments