******.Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Wizara ya Afya unatarajia kuendesha zoezi la utoaji chanjo ya matone kwa ajili ya kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa wa polio, ambapo chanjo hiyo itatolewa kwa watoto wenye umri chini ya miaka 10, kuanzia Agosti 27 hadi Agosti 30, ikiwa ni awamu ya kwanza. Awamu ya pili itaanza Sept 29 hadi Oct 02.2026
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe Albert Chalamila, katika mafunzo hayo ambayo yamefanyika leo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambapo mafunzo yamewahusisha wadau na makundi mbalimbali,
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe Edward Mpogolo, amesema lengo la zoezi hilo ni kuwafikia zaidi ya watoto milioni moja, laki tatu na elfu 37 Mkoani humo, hivyo amewataka wazazi, walezi, viongozi wa Dini, walimu na jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano ili lengo liweze kutimia.
Pia, Mpogolo amesema lengo la kampeni hiyo ya utoaji chanjo ni kuimarisha kinga kwa watoto chini ya umri wa miaka 10, kuzuia kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa polio na kuhakikisha watoto wote ambao hawajapata chanjo toshelevu wanapata huduma hiyo, huku zoezi hilo likipita kwenye maeneo yote yenye mikusanyiko, ikiwemo shuleni, sokoni na kwenye nyumba za ibada.
Aidha, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Mohamed Mang'una, amesema Mkoa huo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya umejipanga kuzifikia takriban shule za msingi 3,675, shule za awali 2,651, vituo vya huduma za afya 344 na nyumba za ibada 3,274, kwa lengo la kuhakikisha watoto wote chini ya umri wa miaka 10 wanafikiwa.
Kwa upande wao, wakuu wa wilaya mbili, ambao ni Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Wakili Albert Msando, na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mikaya Dalmia, pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Matimbwa, wameahidi kushiriki kikamilifu kwenye kampeni hiyo ili kuhakikisha lengo linatimia, huku wakiitaka jamii kuhakikisha watoto chini ya umri wa miaka 10 wanapata chanjo hiyo.












Post a Comment