NA HERI SHAABAN (DARESSALAAM)
MKUU wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo ameziagiza Kampuni za CRJE NA TAISHAN kushirikiana na Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam kumaliza changamoto ya maji taka kata ya Buguruni Kisiwani.
Mkuu wa Wilaya Edward Mpogolo amesema hayo wakati wa ziara ya kikazi kata ya Buguruni ambapo aliziagiza kampuni hizo kutekeleza agizo hilo na kutafuta ufumbuzi ikiwemo ujenzi maalum wa maji taka.
"Nimefanya ziara mimi mwenyewe nimejionea hali ya miundombinu ya maji taka pamoja na athari zinazowakabiri wananchi kutokana na maji kushindwa kupita kwa ufanisi kutokana na mifumo ya maji kuzibwa hapa Buguruni Kisiwani au zimeathiriwa kutokana na shughuli za ujenzi zinazoendelea ikiwemo mfereji uliokuwa unapitisha maji kuelekea mto Msimbazi "amesema Mpogolo.
Mpogolo amesema hali hiyo imepelekea maji kushindwa kupita kwa ufanisi hivyo kurudi katika makazi ya wananchi hivyo amezitaka kampuni hizo kushirikiana na TARURA na Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam kufanya tathimini ya kina kubaini chanzo cha tatizo na kuweka mpango wa pamoja kujenga mfereji wa maji na maji taka kutoka kutoka maeneo ya makazi kwa usalama .
Aidha amesema ujenzi wa mfereji huo unapaswa kuzingatia mahitaji ya sasa pamoja na ukuaji wa makazi katika eneo hilo ili kuhakikisha unakuwa na uwezo kwa kududumia wananchi kwa muda mrefu na kuzuia maji kutuama katika maeneo ya makazi.
Amesema Serikali haitaki kuona wananchi wakiendelea kukumbwa na kero ya maji kila mara huku miundombinu ya Barabara na mazingira yao ikiendelea kuathirika.
Wakati huo huo alizitaka kampuni hizo CRJE NA TAISHAN kwa kushirikiana na TARURA washirikiane Pamoja kwa ajili ya kupata suluhisho endelevu la changamoto ya maji taka katika eneo hilo ili kuondoa athari zitakazojitokeza katika Bonde la SUKITA.




Post a Comment