WANANCHI WA BANGULO WAPONGEZA KUFUTWA HATI NA. 4873 YA SHAMBA LA MIFUGO LA KABIMITA

.........

Na Heri Shaaban,( Dar es Salaam)

WANANCHI wa Bangulo na Pugu Stesheni wamemshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa dhamira yake na upendo wake kwa wananchi uliomfanya kuridhia kufutwa kwa Hati Na. 4873 ya Wizara ya Mifugo, iliyokuwa ikilitambua eneo hilo kama Shamba la Mifugo la Kabimita, hatua inayofungua fursa kwa wananchi kupata haki ya kumiliki ardhi hiyo kihalali.

Akizungumza na wananchi wa Bangulo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema uamuzi huo wa Rais ni hatua kubwa yenye maana ya pekee kwa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi katika eneo hilo wakiwa na changamoto ya uhakika wa umiliki wa ardhi.

 Mpogolo amesema wananchi wanapaswa kumshukuru Rais Dkt. Samia  kwa uamuzi huo, ambao umeonesha dhamira yake ya kusikiliza kilio cha wananchi, kutatua changamoto zao na kuhakikisha wanapata fursa ya kutumia ardhi kama nyenzo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Kwa dhati kabisa, tunamshukuru Rais wetu,. Dkt. Samia . Uamuzi wake wa kufuta Hati Na. 4873 ya Wizara ya Mifugo, iliyokuwa ikifahamika kama Shamba la Mifugo la Kabimita, ni uamuzi mkubwa kwa wananchi wa Bangulo. Tunauona kama ishara ya upendo wake kwa wananchi na dhamira yake ya kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kumiliki ardhi yao kihalali,” amesema  Mpogolo.

Amesema hatua hiyo imeondoa kikwazo kikubwa na sasa wananchi wanapaswa kutumia fursa hiyo kwa kukamilisha taratibu za upimaji, urasimishaji na upatikanaji wa hati miliki ili waweze kuwa wamiliki halali wa ardhi wanayoishi.

“Rais amefungua mlango, sasa ni wajibu wetu wananchi kuutumia tunataka wananchi hawa wawe na hati zao, kwa sababu hati miliki si karatasi tu ni usalama wa ardhi, ni heshima ya umiliki na ni fursa ya mwananchi kutumia mali yake kwa maendeleo, ikiwemo kukopesheka,” amesema.

. Mpogolo amesema eneo hilo, linalohusisha Bangulo na Pugu Stesheni, lina maelfu ya wananchi na zaidi ya kaya 10,000, ambao wamekuwa wakihitaji maeneo yao kupimwa na kurasimishwa.

Aidha amesema kwa sasa ni wananchi takribani 1,000 ambao wamekamilisha malipo yanayohitajika, huku zaidi ya 7,000 wakiwa bado hawajakamilisha taratibu hizo.

Ameziagiza Kamati ya Wananchi wa Bangulo na Pugu pamoja na Diwani wa Kata husika kushirikiana na Serikali katika kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kukamilisha taratibu hizo.

Mpogolo amesema yeye binafsi ataendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha mchakato huo unakamilika, ikiwemo kushirikiana na Wizara ya Mifugo katika kukamilisha taratibu za kubadilisha matumizi rasmi ya eneo hilo.

Ameongeza kuwa changamoto ya eneo hilo si mpya kwake, akieleza kuwa mwaka 2016, wakati akiwa Katibu Tawala, alifika Bangulo akiwa pamoja na Waziri wa Mifugo wa wakati huo, . Luhaga Mpina, na Waziri wa Ardhi wa wakati huo, Hayati  William Lukuvi, kwa ajili ya kushughulikia changamoto ya eneo hilo. 


Mwisho





 

0/Post a Comment/Comments