DIB YAENDELEA KULINDA AMANA ZA WATEJA

.....

Benki tisa zimewahi kuwekwa chini ya ufilisi nchini tangu mwaka 2000, huku baadhi ya michakato yake ikiendelea, Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imeeleza. 

Akizungumza katika Maonesho ya Nane Nane jijini Dodoma, Meneja wa Fedha na Uhasibu wa DIB, Romuli Mtui, amesema benki hizo ni Greenland Bank, Delphi Bank pamoja na benki saba zilizofutiwa leseni mwaka 2017 na 2018, zikiwemo FBM Bank, FDM Bank, Mbinga Community Bank, Njombe Community Bank, Meru Community Bank, Kagera Farmers' Cooperative Bank na Efatha Community Bank.

Mtui amesema mchakato wa ufilisi unaweza kuchukua muda kutokana na taratibu za kisheria, uwepo wa mali, wadai na wadaiwa. Ameongeza kuwa DIB inaendelea kulipa fidia kwa wateja wa benki zilizofungwa na imewataka ambao bado hawajachukua malipo yao, hususan wa FBME Bank, kufuatilia stahiki zao kupitia ofisi za Bodi zilizopo Benki Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam na Dodoma.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa DIB, Lwaga Mwambande, amesema kila mteja mwenye akaunti katika benki yenye leseni ya BoT analindwa na mfumo wa bima ya amana, ambapo kiwango cha juu cha fidia kwa sasa ni Sh milioni 7.5 kwa mwekaji mmoja endapo benki itafutiwa leseni.

Amefafanua kuwa wateja wenye amana zinazozidi kiwango hicho bado wana haki ya kulipwa kupitia mchakato wa ufilisi, huku akibainisha kuwa mfuko wa bima ya amana huchangiwa na benki wanachama kwa asilimia 0.15 ya amana zao kwa mwaka ili kuimarisha uwezo wa kulipa fidia.

Mwambande amesema mbali na kulipa fidia na kusimamia ufilisi, DIB pia husaidia benki zinazokabiliwa na changamoto za kifedha kabla hazijafungwa ili kupunguza hasara na kuimarisha utulivu wa sekta ya fedha nchini.



 

0/Post a Comment/Comments