FEDHA ZA CSR ZA BARRICK NORTH MARA ZAENDELEA KUFANIKISHA MIRADI YA KUBORESHA ELIMU TARIME

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wa pili kulia), akifurahi kuzindua mradi wa jengo la utawala la Shule ya Sekondari Mjini Kati uliotekelezwa kwa fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka mgodi wa Barrick North Mara. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele na viongozi wengine wa wilaya.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akiongozwa na Mwalimu Charles Gibiti kukagua jengo hilo.
Meneja Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi na wafanyakazi wenzake akiwa na baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya Tarime mara baada ya uzinduzi wa ofisi ya utawala katika Shule ya Sekondari ya Mjini kati
Kupitia utekelezaji wa mkakati endelevu wa kampuni na sera za serikali kwa weledi, mgodi wa Barrick North Mara uliopo wilayani Tarime unaendelea kufanikisha miradi mbalimbali kupitia fedha za uwajibikaji wa jamii (CSR), hususani katika sekta ya afya na elimu katika vijiji vinavyozunguka mgodi.

Miradi inayotekelezwa kwa kutumia fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka mgodi wa dhahabu wa North Mara zinaendelea kuboresha mazingira ya kupata elimu, kuongeza ufaulu wa wanafunzi, kuongeza nafasi za wanafunzi wanaojiunga katika shule za msingi na sekondari na kuongeza motisha kwa walimu kutokana na kujengewa ofisi bora na nyumba za kuishi katika wilaya ya Tarime.

Mwishoni mwa wiki walimu waliokuwa wanalazimika kutumia vyumba vya madarasa kama ofisi katika Shule ya Sekondari Mjini Kati iliyopo Nyamongo wilayani Tarime, sasa wamefurahi kupata jengo jipya la ofisi na utawala lenye thamani ya shilingi milioni 172 lililojengwa kwa fedha za CSR ambalo lilizinduliwa rasmi na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa.

Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa Mgodi wa North Mara umetumia shilingi bilioni 26.86 kugharimia utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa jamii (CSR) 255 katika sekta za elimu, afya, barabara, maji, miradi ya kiuchumi na mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime tangu mwaka 2019 ulipoanza kuendeshwa na Barrick kwa ubia na serikali kupitia kampuni ya Twiga.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa mradi huu, Dkt. Bashiru Ally Kakurwa aliuagiza uongozi wa wilaya na halmashauri kuhakikisha linawekewa samani na huduma za umeme na maji ili kuwezesha walimu kutekeleza majikumu ya kiutawala kwa ufanisi.

"Jengo tunalozindua halina samani DC (Mkuu wa Wilaya) jadilianeni na halmashauri, naomba kama Mlezi wa Mkoa [wa Mara], nilichokizundua jipekue muweke maji, samani na umeme, popote nilipozindua yanayotakiwa kukamilishwa yakamilishwe,” aliagiza.

Awali akisoma risala kabla ya uzinduzi Kaimu Mkuu wa shule ya sekondari ya Mjini Kati, Charles Gibiti Pius alisema kabla ya kutekelezwa kwa mradi huu, walimu walikuwa wanatumia vyumba vya madarasa kama jengo la utawala. Mjini Kati ni moja ya shule za sekondari 53 za serikali zilizopo katika Hamashauri ya Wilaya ya Tarime.

Sekta ya elimu inatajwa kuchukua sehemu kubwa ya mabilioni ya fedha za CSR yanayotolewa na mgodi wa Barrick kufadhili miradi ya endelevu ya maendeleo ya jamii katika halmashauri hiyo.

Viongozi mbalimbali, walimu na wanafunzi katika shule zilizopo katika kata zinazozunguka mgodi wameipongeza Barrick kwa uwekezaji wake endelevu.Wanufaika hao wanasema miradi inayoendelea kutekelezwa imefanikisha kuboresha maisha ya wananchi.

Miradi inayotekelezwa kwa kutumia fedha hizo za CSR kutoka mgodi huo inahusisha pia ujenzi wa nyumba za walimu na utengenezaji wa madawati kwa shule za msingi, viti na meza kwa shule za sekondari.

Mapema mwezi huu, kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, alizindua pia vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Matongo ambavyo pia vimejengwa kutokana na fedha za CSR Barrick North Mara.

Miradi hii inayoendelea kuzinduliwa ni sehemu ya miradi mipya 103 ambayo inatekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa fedha za CSR kutoka mgodi wa North Mara.

Mkakati endelevu wa Barrick umejikita zaidi kuleta uendelevu katika shughuli za kampuni kanuni na misingi yake mikuu ikiwa ni: Usalama kwa wafanyakazi wake, uchimbaji madini kwa uwajibikaji, kujenga ushirikiano imara, na kutoa thamani ya muda mrefu ambayo inashirikiwa na washikadau wetu wote.


0/Post a Comment/Comments