*******
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafadh Ameir, amesisitiza nafasi muhimu ya wanawake wanataaluma katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza Agosti 2, 2026 jijini Dar es Salaam katika hafla ya Inclusive Mwalimu Gala 2026, Naibu Waziri amesema kuwa kauli mbiu ya hafla hiyo, “The Contribution of Women Professionals to the Implementation of Tanzania Development Vision 2050”, imeakisi mchango wa wanawake katika kujenga uchumi wa maarifa, ubunifu na teknolojia.
Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu. Hatua zilizotekelezwa ni pamoja na maboresho ya sera na sheria, ujenzi wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji.
Aidha, amesisitiza kuwa mchango wa wanawake hauwezi kupuuzwa na kwamba Serikali ikiendelea kuimarisha usawa wa kijinsia, kuongeza ushiriki wa wanawake katika fani za STEM, kuzuia ukatili wa kijinsia na kuwekeza katika maendeleo ya kitaaluma ya walimu na wahadhiri kupitia mafunzo endelevu na tafiti.
Naibu Waziri ametoa wito kwa walimu, wakufunzi na wahadhiri kuendelea kuwa chachu ya mabadiliko ya Taifa kwa kuandaa kizazi chenye maadili, maarifa na ubunifu.
“Mustakabali wa Taifa upo mikononi mwa vijana na wanafunzi,” amesisitiza, akiwataka kutumia kikamilifu fursa za elimu zinazotolewa na Serikali ili kuleta suluhisho kwa changamoto za kijamii na kiuchumi." amesema Naibu Waziri
Naye Mbunge Viti Maalum, Asha Feruzi, amesema kuwa hafla ya Inclusive Mwalimu Gala 2026 ni jukwaa la kujadili mustakabali wa elimu, ubunifu na teknolojia katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Feruzi amebainisha kuwa matokeo yanayotarajiwa kupitia ushirikiano huo ni kuimarika kwa tafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa, hususan akili unde (Artificial Intelligence). Ameongeza kuwa vyuo vikuu na sekta binafsi vitaunganishwa ili kuzalisha suluhisho, bidhaa na huduma zinazochochea ukuaji wa uchumi shindani na endelevu.







Post a Comment