Na Carlos Claudio, Dodoma.
Shirika la Posta Tanzania limeeleza kuwa utekelezaji wa Mradi wa Huduma Pamoja umeleta mabadiliko makubwa katika upatikanaji wa huduma za Serikali, kwa kuwawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali katika eneo moja bila kulazimika kuzunguka katika ofisi tofauti.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Aicha Nangawe, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Serikali katika Shirika la Posta Tanzania, amesema wazo la kuanzishwa kwa vituo vya Huduma Pamoja lilitokana na utafiti wa upembuzi yakinifu (feasibility study) uliofanyika mwaka 2020, uliobaini kuwa wananchi walikuwa wakipoteza muda na gharama kubwa wakizunguka katika taasisi mbalimbali ili kukamilisha huduma moja.
Amesema hali hiyo ilisababisha Serikali kuanzisha One-Stop Service Centres, zinazolenga kuwawezesha wananchi kupata huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali katika eneo moja, hivyo kupunguza usumbufu, gharama na muda wanaotumia kufuatilia huduma.
“Mradi huu umeleta mabadiliko kwa sababu wananchi sasa wanakuja katika kaunta za Posta na kupata huduma mbalimbali mahali pamoja. Kwa mfano, mwananchi anaweza kupata huduma za NIDA, RITA na huduma nyingine bila kulazimika kusafiri kutoka ofisi moja kwenda nyingine,” amesema Nangawe.
Kwa mujibu wa Nangawe, awali taasisi mbalimbali zilikuwa na madirisha yao ndani ya ofisi za Posta, lakini kupitia Mradi wa Huduma Pamoja, huduma hizo zimeunganishwa katika mfumo mmoja wa kidijitali unaowezesha huduma kutolewa kupitia dirisha moja (single window).
Amesema mfumo huo unatarajiwa kuendelea kuunganishwa na huduma nyingi zaidi za Serikali, hatua ambayo itarahisisha zaidi upatikanaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za umma.
Nangawe amesema pia watumishi wamepewa mafunzo ya kutumia mfumo huo pamoja na namna ya kutoa msaada wa kiufundi ili kuhakikisha mfumo unaendelea kufanya kazi kwa ufanisi.
Aidha, amesema watumishi wamepatiwa mafunzo kuhusu mfumo wa call centre, unaowawezesha kupata msaada pale wanapokutana na changamoto wakati wa kutoa huduma.
Akizungumzia mafanikio ya mradi huo, Nangawe amesema tangu kuanza kwa huduma hizo, zaidi ya wananchi laki tatuwamekwishahudumiwa katika ofisi zinazotekeleza huduma hiyo.
Amesema miongoni mwa huduma zinazohitajika zaidi ni huduma za Vitambulisho vya Taifa (NIDA), huku Shirika la Posta likiendelea kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo kwa urahisi kupitia vituo vilivyoanzishwa.
“Tumeshuhudia mapato yakiongezeka kupitia huduma zinazotolewa, kwa sababu wananchi wengi wamekuwa wakifika katika ofisi zetu kupata huduma. Serikali nayo imeweza kupata mapato kupitia huduma zinazotolewa katika kaunta hizi,” amesema.
Amesema kwa sasa utekelezaji wa mradi huo umeanza kama mradi wa majaribio (pilot) katika maeneo ya Dar es Salaam na Dodoma, huku Shirika la Posta likilenga kuupanua nchini kote.
Ameongeza kuwa, baada ya huduma nyingi zaidi kuunganishwa katika mfumo wa single window na mradi kufikia utekelezaji wa kitaifa, wanatarajia Serikali kuongeza zaidi mapato na wananchi kupata huduma kwa ufanisi mkubwa.
Nangawe amesema mwitikio wa wananchi katika maeneo ambayo huduma hiyo tayari inaanza kutolewa umekuwa mzuri, akibainisha kuwa vituo hivyo vimekuwa vikitembelewa na wananchi wanaohitaji huduma mbalimbali.
Amesema hali hiyo inaonesha kuwa wananchi wameupokea mradi huo kwa matarajio makubwa kutokana na umuhimu wake katika kurahisisha upatikanaji wa huduma za Serikali.
Katika hatua nyingine, Nangawe amesema mradi huo umezingatia pia mahitaji ya watu wenye ulemavu na mahitaji maalum, kwa kuhakikisha wanapata huduma katika mazingira rafiki na yanayofikika.
Amesema katika ofisi 32 zilizofanyiwa ukarabati kupitia mradi huo, zimewekewa miundombinu rafiki ikiwemo rampu na kaunta maalum kwa ajili ya kuwahudumia watu wanaotumia viti vya magurudumu.
“Katika ofisi zetu zote 32 zilizofanyiwa ukarabati kuna rampu kutoka mlangoni na kuna kaunta maalum kwa ajili ya kuwahudumia watu wenye mahitaji maalum. Huduma wanazopata zinazingatia mahitaji yao,” amesema.
Nangawe amewataka wasimamizi wa mradi kuendelea kuutazama kwa upana zaidi na kuwahusisha wawekezaji ili huduma hizo ziweze kusogezwa karibu zaidi na wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema uwekezaji zaidi utasaidia kuongeza idadi ya vituo vya Huduma Pamoja, kuunganisha huduma nyingi zaidi za Serikali katika mfumo mmoja na hatimaye kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi bila kusafiri umbali mrefu.
“Tunawashukuru kwa hatua ambayo mradi umefikia, lakini tunashauri endapo tutapata wawekezaji zaidi, tuweze kufikiriwa ili huduma hizi ziweze kuwafikia wananchi karibu zaidi,” amesema.



Post a Comment