KODI ZACHOCHEA MAENDELEO KUSINI PEMBA

*******
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba,  Rashid Hadidi Rashid, amesema katika siku za karibuni mkoa huo umepiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kasi, hali ambayo imetokana na kodi zinazolipwa na wananchi kwa ajili ya maendeleo yao.

Ametoa kauli hiyo Agosti 11, 2026, alipotembelewa ofisini kwake Kisiwani Pemba na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda.

Mhe. Rashid amesema hivi sasa Kisiwani Pemba kumekuwa na mageuzi makubwa ya miundombinu ya barabara, elimu na afya kutokana na kuhamasika kwa wananchi katika ulipaji wa kodi.

Amesema kuboreshwa kwa huduma za kijamii Kisiwani humo kumeendelea kuwavutia zaidi wawekezaji, ambao nao wamekuwa wakiongeza mapato ya kodi kupitia uwekezaji wao.

Amesema Serikali ya Mkoa wa Kusini Pemba imekuwa ikishirikiana na TRA kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuendelea kulipa kodi, na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo wenye tija kwa maendeleo ya wananchi.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, amemshukuru Mkuu huyo wa Mkoa kwa kushirikiana na TRA kutoa elimu ya kodi kwa wananchi, huku akiwashukuru walipakodi kwa kuendelea kuiamini TRA na kulipa kodi kwa hiari.

Amesema TRA itaendelea kutoa huduma bora za kodi kwa wananchi kwa kuwasikiliza na kutatua changamoto zao, huku ikiwezesha biashara zao kupitia dawati la uwezeshaji biashara linaloratibiwa na Mamlaka hiyo.




 

0/Post a Comment/Comments