Na Carlos Claudio, Dodoma.
Kampuni ya Kuja na Shoka Tools Manufacturing ya Tabora imefanikiwa kusambaza na kufunga mashine za uzalishaji wa mkaa banda katika magereza 61 na vikosi 22 vya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa miradi inayolenga kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi wa Tanzania Clean Cooking Program (TCCP), Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Leonard Gabriel Shoka, amesema msaada uliotolewa kupitia African Enterprise Challenge Fund (AECF) umeiwezesha kampuni hiyo kuwafikishia wanufaika teknolojia ya uzalishaji wa mkaa banda pamoja na kuwapatia mafunzo ya matumizi na uzalishaji.
Amesema teknolojia hiyo imekuwa muhimu katika kuwasaidia wanufaika kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa wa kawaida, huku wakiweza kuzalisha mkaa banda kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo yao.
“Mradi huu umetuwezesha kufunga mashine katika vikosi 22 vya JKT na magereza 61, pamoja na kutoa mafunzo ya uzalishaji ili waweze kujitegemea na kuacha kabisa matumizi ya kuni na mkaa,” amesema Shoka.
Hata hivyo, Shoka amesema changamoto kubwa inayokabili kampuni zinazojihusisha na nishati safi ya kupikia ni upatikanaji wa mitaji kutoka taasisi za fedha, hali ambayo inaweza kuchelewesha upanuzi wa teknolojia hiyo nchini.
Amesema licha ya kampuni kuwa na mikataba ya utekelezaji wa miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni moja, baadhi ya taasisi za fedha zimekuwa zikisita kutumia mikataba hiyo kama dhamana ya kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi.
Kutokana na hali hiyo, ameiomba Serikali kuangalia kwa karibu changamoto ya upatikanaji wa fedha katika sekta ya nishati safi ili taasisi za fedha ziweze kushiriki kikamilifu katika kuchochea uwekezaji na upanuzi wa teknolojia hizo.
“Biashara hizi bila support ya benki hatuwezi kufika mbali. Tunaona impact kubwa inayotokea katika jamii, lakini upande wa mabenki bado umekuwa changamoto. Tunaomba Serikali iangalie suala hili ili miradi ya nishati safi iweze kufikia malengo yaliyowekwa,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa Programu wa Tanzania Clean Cooking Program (TCCP), Frederick Tunutu, amesema mpango huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uwezo wa kampuni zinazofanya biashara ya nishati safi, hususan katika kuwafikia wananchi wa maeneo ya vijijini.
Amesema TCCP ulioanza mwaka 2022 ulilenga kujenga uwezo wa kampuni kupitia ruzuku ili ziweze kuzalisha na kusambaza teknolojia za nishati safi katika maeneo ambayo kwa muda mrefu hayakuwa yamefikiwa kikamilifu.
“Makampuni mengi yalikuwa yamejikita mijini, lakini tulijaribu kuhakikisha kupitia ruzuku wanakwenda pia vijijini,” amesema Tunutu.
Kwa mujibu wa Tunutu, mpango huo ulikuwa na lengo la kusaidia kampuni 15, lakini hadi sasa kampuni 13 zimefanikiwa kupata ruzuku.
Amesema mradi huo uliweka lengo la kuwafikia watu 60,000, lakini umevuka matarajio kwa kuwafikia zaidi ya watu 180,000, huku taasisi mbalimbali zikiwemo shule na vyuo zikifaidika na teknolojia hiyo.
Amesema jumla ya majiko 900 yamesambazwa katika shule mbalimbali, huku mradi huo ukiwa umefadhiliwa kwa kiasi cha dola za Marekani milioni 4.9.
Tunutu amesema kampuni ndogo zilipatiwa ruzuku kuanzia dola 50,000, huku kampuni kubwa zikipata hadi dola 200,000 kulingana na mahitaji na ukubwa wa miradi.
Amesema mafanikio hayo yanaonesha kuwa sekta ya nishati safi ya kupikia inaendelea kukua, huku kampuni nyingi zaidi zikianza kuwekeza katika uzalishaji na usambazaji wa teknolojia hizo.
Naye Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia katika Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay, amesema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, ikiwemo kuongeza upatikanaji wa teknolojia na kutoa ruzuku kwa wananchi.
Amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutoa ruzuku kwa bidhaa za nishati safi ya kupikia ili kuzifanya zipatikane kwa wananchi wengi zaidi.
Kwa mujibu wa Wizara, zaidi ya majiko banifu 200,000 yanasambazwa nchini kwa bei ya ruzuku inayofikia takribani asilimia 85, hatua inayolenga kupunguza gharama kwa wananchi na kuwahamasisha kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.
Aidha, Serikali inaendelea na mpango wa kusambaza zaidi ya majiko ya gesi 400,000 yenye mitungi ya kilo sita kwa bei ya ruzuku, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza matumizi ya gesi katika maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakitegemea nishati chafu.
Serikali pia inahamasisha matumizi ya umeme kama moja ya vyanzo vya nishati safi ya kupikia, huku TANESCOikiendelea na mfumo wa on-billing unaowawezesha wananchi kupata majiko ya umeme na kulipia gharama zake kupitia bili ya umeme.
Wizara imesisitiza kuwa nishati safi ya kupikia si gesi pekee, bali inajumuisha umeme, biogas, briquettes pamoja na teknolojia nyingine salama na zenye ufanisi.
Aidha, Serikali imeeleza kuwa baadhi ya kampuni zimeanza kutumia mifumo ya Pay-As-You-Go, inayowawezesha wananchi kupata vifaa vya kupikia na kulipia kwa awamu, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya gharama kubwa za awali.
Kwa mujibu wa Serikali, mikakati hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wa mijini na vijijini wanapata nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu, huku kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa kukisaidia kulinda mazingira na kuboresha afya na maisha ya wananchi.
Tunutu amesema mafanikio ya mpango huo yanaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, wafadhili, mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi, taasisi za fedha na wananchi katika kufanikisha ajenda ya taifa ya nishati safi ya kupikia.
Amesema kipaumbele kinachofuata ni kuongeza kasi ya usambazaji wa teknolojia hizo vijijini, ambako matumizi ya kuni na mkaa bado ni makubwa kutokana na changamoto za upatikanaji na gharama za teknolojia mbadala.
Kwa ujumla, juhudi hizo zinaendelea kuimarisha ajenda ya Tanzania ya kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kupunguza utegemezi wa nishati zinazochafua mazingira, huku sekta binafsi ikipewa nafasi kubwa ya kuwa sehemu ya suluhisho.




Post a Comment