Mwenyekiti wa huduma ya The Healing Missionaries (THM), Papa Mlunda, amesema maandalizi ya Tamasha la Sebene Gospel Festival Season 2 yamekamilika huku akieleza kuwa tamasha hilo limekua kwa kiwango kikubwa tangu kuanzishwa kwake.
Amesema mafanikio ya msimu wa kwanza uliofanyika Sinza Mori na kuhudhuriwa na zaidi ya waumini 2,000 yamechochea maandalizi makubwa zaidi mwaka huu kwa lengo la kuhubiri Injili kupitia sifa na kuabudu.
Papa Mlunda amesema tamasha hilo litafanyika Agosti 7 hadi 8 na limevuka mipaka ya Tanzania kwa kuwakutanisha waimbaji na watumishi wa Injili kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo Olivia Kalabasi kutoka Ufaransa, Fistombo na Alkambomba kutoka DRC, Alice Kimanzi kutoka Kenya pamoja na Kings Malembe kutoka Zambia.
Msimamizi wa tamasha hilo, MC Nsena, amesema maandalizi yamekamilika na waumini wote watahudhuria bila kiingilio, huku akieleza kuwa kutakuwa na ibada za usiku kucha, mafundisho ya Neno la Mungu, maombi na huduma mbalimbali za kiroho.
Amesema shughuli zitaanza mapema asubuhi ambapo wafanyabiashara watapata nafasi ya kutangaza bidhaa zao bila malipo, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki tukio hilo la injili pamoja na familia na marafiki zao.
Naye msanii wa muziki wa Injili kutoka Nairobi, Kenya, Alice Kimanzi, amesema ana heshima kubwa kushiriki tamasha hilo, akieleza kuwa mazoezi yaliyofanyika yameonyesha kiwango cha juu cha uimbaji na upigaji wa vyombo vya muziki.
Amesema matarajio yake ni kuona watu wengi wakijitokeza kushiriki ibada ya sifa na kuabudu, akisisitiza kuwa kila kitu kimeandaliwa vizuri kwa ajili ya kumtukuza Mungu.
Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Huduma za Vijana kutoka CRDB Bank, Mshindo Magimba, amesema benki hiyo imefurahi kupata mwaliko kutoka THM na kuliona tamasha hilo kama fursa kubwa kwa vijana kupata elimu ya fedha.
Amesema CRDB itatumia jukwaa hilo kuwapatia vijana elimu ya kuweka akiba, kupanga mipango ya baadaye na kuwafahamisha huduma mbalimbali za kifedha ikiwemo Sim Banking, Lipa Namba na matumizi ya POS kwa wafanyabiashara na wageni watakaohudhuria.



















Post a Comment