Taasisi ya Madina Foundation imeendelea kutoa msaada kwa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, ambapo imelipia bili za matibabu za wagonjwa 10 wenye changamoto za kifedha.
Malipo hayo ya Shilingi milioni moja yamefanyika leo wakati wa ziara ya kila mwezi ya Madina Foundation katika hospitali za rufaa nchini, ziara zinazolenga kuwafikia wagonjwa wanaohitaji msaada wa matibabu na mahitaji mengine muhimu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Madina Foundation, Sarah Abdallah Hamisi, amesema taasisi hiyo imekusanya Shilingi milioni 15,220,629 katika mwezi huu, huku Shilingi milioni 8,566,234 zikitumika kuwahudumia wagonjwa 139.
Sarah amesema kwa mwaka, taasisi hiyo huwasaidia wagonjwa takribani 1,200, huku kipaumbele kikubwa kikiwa ni kugharamia matibabu kwa wagonjwa ambao wanashindwa kumudu gharama za huduma za afya.
Amesema kwa wagonjwa wanaopatiwa matibabu Ocean Road, mahitaji makubwa yapo katika kugharamia matibabu kutokana na aina ya huduma wanazohitaji, hivyo msaada wa kifedha ni muhimu katika kuwawezesha kuendelea na matibabu.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Ocean Road, Karafuu Yusuph, amesema Madina Foundation imekuwa mshirika muhimu wa hospitali hiyo katika kuwasaidia wagonjwa wenye uhitaji.
Yusuph amesema ushirikiano huo ambao umedumu kwa takribani miaka mitano umesaidia wagonjwa wengi kupata huduma muhimu, hasa wale ambao uwezo wao wa kifedha hauwaruhusu kugharamia matibabu wenyewe.
Mbali na malipo ya bili za matibabu, Madina Foundation imekabidhi pia mahitaji ya chakula na usafi yenye thamani ya Shilingi milioni 1.327, yakiwemo sukari, sembe, ngano, sabuni na pampers.
Madina Foundation imekuwa ikifanya shughuli za kijamii tangu mwaka 2021 na kwa sasa ina wanachama zaidi ya 4,300 wanaochangia sadaka na michango kwa ajili ya kusaidia wagonjwa pamoja na jamii kwa ujumla.













Post a Comment