Na Carlos Claudio, Dodoma.
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imewahimiza wananchi, hususan wakulima, kutumia Mfumo wa Anwani za Makazi kwa kuwa unarahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma nchini.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi wa Anwani za Makazi kutoka Wizara hiyo, Mhandisi Edith Turuka, wakati wa Maonesho ya 33 ya Wakulima (Nanenane 2026) yanayoendelea katika Viwanja vya Maonesho ya Kilimo vya Dkt. John Samuel Malecela.
Mhandisi Turuka amesema wizara inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa, ikiwemo usalama wa mtandao, mifumo ya kidijitali ya Serikali na Mfumo wa Anwani za Makazi, ambao umeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuunganisha watoa huduma na wananchi.
Amesema kupitia banda la Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, wananchi wanapata fursa ya kujua anwani zao za makazi, kusahihisha taarifa za anwani pamoja na kupata huduma mbalimbali zinazotolewa kupitia mfumo huo wa kidijitali.
"Mfumo wa Anwani za Makazi ni msingi muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma. Unarahisisha mawasiliano kati ya mtoa huduma na mpokeaji wa huduma, huku ukiongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za Serikali na sekta binafsi," amesema.
Aidha, amesema wananchi wanaweza kupata huduma ya barua ya utambulisho wa makazi kwa njia ya kidijitali, kutambua maeneo ya huduma muhimu yaliyopo karibu nao na kushirikisha anwani zao kwa taasisi au wadau wanaowahudumia.
Kwa upande wa sekta ya kilimo, Mhandisi Turuka amesema mfumo huo unawasaidia wakulima kupokea bidhaa na huduma kwa urahisi zaidi, kwa kuwa anwani sahihi huwezesha pembejeo za kilimo, vifaa na huduma nyingine kufikishwa moja kwa moja katika maeneo husika.
Ameongeza kuwa mfumo huo pia unawawezesha wakulima kutambua maeneo yanayotoa huduma muhimu kama vile pembejeo za kilimo, huduma za ugani na huduma nyingine zinazochangia kuongeza tija katika uzalishaji.



Post a Comment