MHE. CHANDE AHIMIZA UHIFADHI WA MISITU KUKUZA SEKTA YA KILIMO, UVUVI NA UFUGAJI

............

Na Saidi Lufune, Dodoma

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) amewataka wadau na taasisi binafsi kushirikiana na Serikali katika jukumu la kulinda na kuhifadhi rasilimali za misitu ili kusaidia ukuaji wa sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji kwa maslahi mapana ya maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Mhe. Chande amesema hayo leo Agosti 6, 2026 katika Viwanja vya Maonesho ya Nane Nane Nzuguni jijini Dodoma alipotembelea Maonesho ya 33 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini ambapo amesisitiza kuwa maendeleo ya sekta hizo yanatokana na kuimarika kwa shughuli za uhifadhi wa misitu na vyanzo vya maji vilivyopo hapa nchini.

“Hatuwezi kuwa na kilimo bora kama hakuna uhifadhi bora ama hatuwezi uhifadhi katika nchi yetu, hatuwezi kuwa na ufugaji bora kama hatuna uhifadhi katika nchi yetu, hatuwezi kuwa na maisha bora kama hatuna uhifadhi katika nchi yetu. Kwa hiyo tuendelee kushirikiana katika kuhifadhi rasilimali zetu ikiwemo misitu, vyanzo vya maji ili tuwe na matokeo mazuri kwenye kilimo chetu, ufugaji wetu na maisha yetu,” alisema Mhe. Chande.

Katika hatua nyingine Mhe. Chande amewasihi washiriki wa Maonesho hayo kuitafsiri na kuitekeleza kwa vitendo Kaulimbiu ya Maonesho hayo kwa mwaka huu; 'Tambua Soko, Ongeza Tija Kuelekea Dira 2050' kwa kuongeza ubora na thamani ya bidhaa zao mara baada ya kutambua masoko ya ndani na nje ya nchi katika kutekeleza na kufikia malengo ya Serikali na Dira ya 2050.

“Ukishalitambua soko unatakiwa kuongeza tija, na ninaamini kabisa taasisi zetu zote za umma na binafsi zitaifanyia kazi ni muhimu sana kuzingatia na kuiweka kichwani na kwenda kuifanyia kazi na isibakie tu kwenye 'slogan', tumetambua masoko mara kadhaa, tunasisitiza kwenye biashara bahati mbaya kwenye mauzo tulikua tumesahau kidogo, natamani iende kufanyiwa kazi kwa vitendo,” alisistiza Mhe. Chande.

Aidha, amewataka waoneshaji na watazamaji wa Maonesho hayo kuwa wazalendo na mabalozi wazuri katika kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kuongeza tija na thamani ya ongezeko la watalii kutoka ndani na nje ya nchi kupitia mazao mapya ya utalii.

“Nitoe mwito kwa wananchi kila mmoja awe Balozi wa kutangaza utalii wa nchi yetu, tunavyo vyanzo vingi, tunavyo vivutio vingi, tuvifanyie kazi kwa sababu hata kilimo ni sehemu ya utalii, kwa hiyo kila mmoja awe Balozi wa kutangaza vivutio vyetu na bidhaa zetu tulizo nazo kwa maslahi yetu wenyewe na taifa kwa ujumla,” alisisitiza Mhe. Chande.

Vile vile, Mhe. Chande alimshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na Maonesho hayo kuendelea kuwa bora kila mwaka ikiwa ni kutokana na juhudi na utayari wake wa vitendo, kifedha na mawazo yake anayoendelea kuyatoa katika kujenga taifa.






 

0/Post a Comment/Comments