MIAKA 40 KUTOKA ZERO HADI UBUNIFU MAGANDA YA KOROSHO SASA NI PESA

......

Na Ester Maile TANGA

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH), Amos Nungu, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, ili kujifunza bunifu mbalimbali na kununua bidhaa zinazozalishwa na wabunifu wazawa kwa lengo la kuunga mkono juhudi zao.

Nungu amesema maonesho hayo yamekusanya bunifu mbalimbali zinazooneshwa katika Banda la COSTECH na mabanda ya taasisi nyingine, akisisitiza kuwa Tanzania ina watafiti na wabunifu wenye uwezo mkubwa ambao wanafanya kazi zinazolenga kutatua changamoto za jamii na kuongeza thamani katika sekta mbalimbali za kiuchumi.

Amesema miongoni mwa bunifu alizoziona katika maonesho hayo ni teknolojia ya ufuatiliaji wa afya ya mifugo, ambapo mbunifu ametengeneza kifaa kinachowekwa kwenye sikio la ng’ombe na kusaidia kufuatilia mwenendo wa afya ya mnyama. Kwa mujibu wa Nungu, ubunifu huo unaonesha namna teknolojia inavyoweza kutumika kuboresha uzalishaji wa mifugo na kusaidia wafugaji kufanya maamuzi kwa wakati.

Ameitaja pia bunifu inayofanywa katika Taasisi ya  Nelson Mandela African Institution of Science and Technology, ambapo mbunifu aliyewahi kufadhiliwa na COSTECH miaka mitano iliyopita ametumia maganda ya korosho kutengeneza bidhaa ya kulainisha ngozi. 

Nungu amesema ubunifu huo umeendelea kukua na sasa umefikia hatua ya kuwa na kiwanda ndani ya chuo hicho, hatua inayodhihirisha umuhimu wa uwekezaji katika tafiti na ubunifu.

Aidha, amesema COSTECH imekuwa ikiwekeza katika bunifu za akili unde (Artificial Intelligence) na miaka minne iliyopita ilifadhili bunifu katika maeneo mbalimbali, hatua ambayo imewezesha kuibuka kwa matumizi ya teknolojia hiyo katika kutatua changamoto za jamii. Miongoni mwa matokeo hayo ni programu tumizi inayosaidia kutambua magonjwa ya samaki, hususan katika ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba (cage farming).

Akizungumza kuhusu mwelekeo wa COSTECH kuelekea maadhimisho ya miaka 40 ya taasisi hiyo, Nungu amesema wataendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu kupitia ufadhili, mijadala na majadiliano yatakayosaidia kutathmini walikotoka na wanakokwenda.

 

0/Post a Comment/Comments