Na Mwandishi wa OTR
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) Jumanne, Agosti 11, 2026, ilifanya mazungumzo na kampuni ya Fitch Ratings Ltd ikiwa ni sehemu ya mapitio ya pili ya mwaka 2026 ya tathmini ya Fitch Ratings, katika mchakato unaohusisha taasisi mbalimbali za Serikali.
Mazungumzo hayo yanalenga kuwapa wachambuzi wa Fitch Ratings fursa ya kupata taarifa za kina kuhusu mwenendo wa uchumi wa Tanzania, utekelezaji wa sera za kibajeti na fedha, pamoja na mikakati ya Serikali katika usimamizi wa deni la Taifa.
Kwa upande wa OTR, mjadala ulijikita katika utendaji wa taasisi za umma, mageuzi yanayoendelea, vihatarishi vya kifedha, pamoja na mtiririko wa fedha kati ya Serikali na taasisi za Umma.
Mapema mwaka huu, Fitch Ratings iliendelea kuipa Tanzania daraja ‘B+’ kwa hadhi ya ulipaji wa madeni ya muda mrefu ya fedha za kigeni, ikitaja mwelekeo imara wa ukuaji wa uchumi na uwezo wa Serikali kukabiliana na changamoto za kifedha baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Fitch inakadiria kuwa uchumi wa Tanzania utakua kwa asilimia 6 kwa mwaka 2026, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi ya wastani wa asilimia 4.5 kwa nchi zenye daraja la ‘B’.
Katika muktadha huo, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, aliyeongoza timu ya OTR, aliieleza timu ya Fitch kuhusu mageuzi yanayolenga kuboresha utendaji na ufanisi wa taasisi za umma, kuimarisha utawala bora na uwajibikaji, pamoja na kupunguza utegemezi wa taasisi hizo kwa Serikali.
Alisema ajenda ya mageuzi ya OTR katika kipindi cha miaka miwili iliyopita imeweka mkazo zaidi katika uongozi, usimamizi wa utendaji na uwajibikaji, ikiwemo kuboresha ubora wa Bodi na timu za menejimenti na kuimarisha tathmini za Bodi ili kubaini mapungufu ya ujuzi.
Bw. Mchechu alisema matokeo ya mageuzi hayo yanaendelea kuonekana katika mchango wa kifedha wa taasisi za umma kwa Serikali.
Katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2026, taasisi zilizo chini ya Msajili wa Hazina zilichangia takribani Sh1.881 trilioni kwa Serikali kupitia gawio na michango mingine, ikilinganishwa na Sh1.028 trilioni katika mwaka wa fedha uliotangulia.
“Tunachokiona ni utayari wa taasisi kuanza kuchangia, au kuongeza mchango wao kwa Serikali,” alisema Bw. Mchechu.
Aliongeza kuwa taasisi zinazoendelea kuhitaji msaada wa Serikali zinatarajiwa kuonesha namna zinavyopunguza utegemezi huo.
Alisema hatua za urekebishaji na uwekezaji wa mtaji zilizochukuliwa katika taasisi kama Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) zimesaidia kupunguza majukumu hayo na kuimarisha hali ya kifedha ya taasisi hizo.
Timu ya Fitch pia iliomba taarifa kuhusu mipango ya kuorodhesha baadhi ya taasisi za umma katika soko la mitaji.
Bw. Mchechu alisema Benki ya Biashara Tanzania (TCB) ni miongoni mwa taasisi zinazotayarishwa kuorodheshwa katika soko la mitaji kupitia uuzaji wa hisa kwa umma kwa mara ya kwanza (IPO), huku Shirika la Taifa la Bima (NIC) likifanyiwa tathmini kwa ajili ya uwezekano wa kuorodheshwa katika soko hilo.
Lengo la muda mrefu ni kurekebisha, kuimarisha na kuorodhesha katika soko la mitaji taasisi kadhaa za umma zinazofaa kabla ya mwaka 2030.
Bw. Mchechu alisema pia OTR imezipa taasisi 58 za umma uhuru zaidi wa kiutendaji, unaoziruhusu kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mamlaka walizopewa bila kuingiliwa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Alisema mageuzi hayo yameimarisha pia uwezo wa ndani wa OTR, hususan katika uchambuzi wa biashara, na hivyo kuiwezesha Ofisi kufanya uchambuzi wa kina zaidi wa bajeti, uwekezaji na mipango ya kimkakati ya taasisi za umma.
Msajili wa Hazina alisema ushirikiano kati ya OTR na Wizara zinazosimamia sekta mbalimbali umeimarika, huku uhusiano huo ukielekezwa zaidi katika kuhakikisha taasisi za umma zinatekeleza vipaumbele vya Serikali.
“Si suala tena la kusema ‘unapaswa kufanya hili na si lile’, bali ‘unafanyaje ili taasisi hii itekeleze kile ambacho Mhe. Rais anataka?’” alisema Bw. Mchechu.
Ujumbe wa Fitch uliongozwa na Bw. José Mantero, Mkurugenzi Mshirika na mchambuzi mkuu anayeshughulikia Tanzania, akifuatana na Bi. Gaimin Nonyane, Mkurugenzi wa Kitengo cha Sovereign and Supranational Group cha Fitch Ratings, na Bw. Gerard Arabian, Makamu wa Rais na Mshauri wa Masuala ya Serikali ‘Sovereign Advisor’ katika Kitengo cha Public Sector Group Corporate Banking.
Bw. Mantero alisema Fitch ililenga kupata uelewa mpana zaidi kuhusu ajenda ya mageuzi ya OTR katika mashirika ya umma, hususan juhudi za kuboresha utendaji wa taasisi na kusimamia madeni na mtiririko wa fedha kati ya Serikali na taasisi za umma.
Alisema mapitio hayo pia yanatathmini athari za maendeleo yanayoendelea katika Mashariki ya Kati kwa Tanzania, ikiwemo athari zinazoweza kujitokeza katika fedha za Serikali, urari wa malipo na mfumuko wa bei kutokana na mabadiliko ya bei za mafuta na mbolea.
Akizungumzia hali chanya ya kifedha ya Serikali inayotokana na uhusiano wake wa kifedha na taasisi za umma, Bw. Mantero alisema: “Hii ni habari njema sana kwa hali ya fedha za Serikali.”
Kwa upande wake, Bi. Nonyane alionekana kuvutiwa na kuongezeka kwa mchango wa mashirika ya umma, akibainisha kuwa mchango huo wa hivi karibuni ulikuwa sawa na takribani asilimia 0.8 ya Pato la Taifa.
Alitaka pia kufahamu namna hali hiyo ilivyobadilika kutoka kipindi ambacho baadhi ya mashirika ya umma nchini yalikuwa yakikabiliwa na changamoto za kifedha.
Mwelekeo huo unaongeza matumaini kwamba mageuzi yanayoendelea yataimarisha zaidi utendaji na uendelevu wa kifedha wa taasisi za umma, kuongeza mchango wao katika uchumi na mapato ya Serikali, pamoja na kuunga mkono juhudi pana za Tanzania za kudumisha uimara wa kifedha na kuboresha hadhi yake ya mikopo.
Taarifa zilizotolewa katika mazungumzo ya OTR na Fitch Ratings yatachangia katika tathmini pana ya kampuni hiyo kuhusu uwezo wa Tanzania wa kutimiza majukumu yake ya kifedha, ikiwa ni sehemu ya mapitio ya pili ya mwaka 2026 ya tathmini ya hadhi ya Tanzania ya ulipaji wa madeni ya Serikali.






Post a Comment