MVUA KUBWA ZA EL NINO ZAJA OCTOBA-TM

...............
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imezitaka mamlaka zinazohusika na miundombinu ya usafiri, ikiwamo reli, kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za Vuli zinazotarajiwa kuwa juu ya wastani hadi wastani katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026. 

TMA imesema msimu huo wa mvua unatarajiwa kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu, hali inayoweza kusababisha mvua za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani ya kaskazini, nyanda za juu kaskazini mashariki, ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma. 

Kwa mujibu wa TMA, mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya Septemba na wiki ya kwanza ya Oktoba 2026 katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, kabla ya kusambaa taratibu katika maeneo mengine ndani ya mwezi Oktoba. 

Akitoa utabiri huo leo, Agosti 18, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Ladislaus Chang'a, amesema vipimo vya joto la bahari katika eneo la Niño 3.4 vilifikia nyuzi joto 2.2 mwezi Agosti na vinatarajiwa kuongezeka hadi nyuzi joto 3.6 ifikapo Desemba.

 Amesema hali hiyo inaweza kuongeza uwezekano wa kutokea kwa mvua kubwa zinazoambatana na upepo mkali na mafuriko katika baadhi ya maeneo, hali inayoweza kuathiri sekta mbalimbali, hususan miundombinu ya usafiri. 

Ameeleza kuwa reli ya mwendokasi (SGR), reli ya kawaida (MGR), barabara na madaraja pamoja na shughuli za bandari ni miongoni mwa maeneo yanayoweza kuathirika kutokana na mmomonyoko wa udongo na mafuriko. 

TMA imesisitiza umuhimu wa mamlaka husika kuchukua hatua za mapema ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.



0/Post a Comment/Comments