Na Ester Maile TANGA
Francis Antony Madanganya, Mkufunzi kutoka Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Chang’ombe jijini Dar es Salaam, ambaye ni mlemavu wa viungo, ameonyesha ubunifu wa Power Bank yenye uwezo wa kuchaji laptop hadi kufikia asilimia 100, akisema ubunifu huo ni sehemu ya jitihada za kuthibitisha kuwa ulemavu si kikwazo kwa mtu mwenye dhamira ya kutumia ujuzi kutatua changamoto za jamii.
Madanganya ameonyesha ubunifu huo katika maadhimisho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, ambapo amesema amejivunia kuwa miongoni mwa wabunifu walioweka mkazo katika kutengeneza Power Bank inayoweza kuchaji laptop, tofauti na Power Bank nyingi zinazotumika zaidi kuchaji simu.
Amesema safari ya kufikia hatua hiyo haikuwa rahisi kutokana na changamoto alizokutana nazo katika maisha yake akiwa mtu mwenye ulemavu wa viungo, lakini hakukata tamaa na badala yake alitumia ujuzi alioupata VETA kuendeleza ndoto yake ya ubunifu.
“Pamoja na changamoto nilizokutana nazo, niliamua kupambana na kuhakikisha nafikia ndoto yangu. Walimu wangu VETA wamenipa ujuzi ambao leo nautumia kubuni na pia kutoa elimu ya ubunifu kwa wengine,” amesema Madanganya.
Ameongeza kuwa katika mchakato wa kutengeneza Power Bank hiyo alipata msaada wa vifaa kutoka kwa walimu wake pamoja na baadhi ya watu waliomuunga mkono, huku akiiomba Serikali na jamii kwa ujumla kuwapa nafasi na kuwaunga mkono watu wenye ulemavu wenye vipaji na uwezo wa kubuni bidhaa zinazoweza kuwa na manufaa kwa jamii.
“Naomba Serikali na jamii wanisaidie mtaji wa shilingi milioni 10 ili niweze kununua vifaa vinavyohitajika kutengeneza Power Bank hizi kwa wingi, kisha niziuze ili nijiongezee kipato na pia niendelee kubuni bidhaa nyingine,” amesema.








Post a Comment