MZUMBE YATOA ONYO KWA MATUMIZI YA AI KATIKA TAASISI ZA SERIKALI

.....

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Chuo Kikuu Mzumbe kimewataka watumishi wa taasisi za Serikali kuwa makini katika matumizi ya teknolojia za akili bandia (AI), hususan wanaposhughulikia taarifa nyeti zinazohusu taasisi na usalama wa nchi.


Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe anayeshughulikia Taaluma, Tafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui Petro, wakati wa kufunga mradi wa DATA2INFO.

Prof. Tundui amesema pamoja na umuhimu na faida zinazopatikana kupitia matumizi ya AI, kuna haja ya kuweka mipaka na miongozo inayoeleza aina ya taarifa zinazoweza kuingizwa kwenye mifumo hiyo, hasa kwa watumishi wanaofanya kazi katika taasisi za Serikali.

“Lazima kuwe na limitation ya nini cha kumpa AI na nini nisimpatie AI inapofika katika suala la usalama wa taarifa za nchi,” alisema Prof. Tundui.

Amesema watumiaji wanapaswa kutambua kuwa wanapoweka taarifa katika baadhi ya mifumo ya AI, wanapaswa kuzingatia hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na namna taarifa hizo zinavyoweza kuchakatwa na kuhifadhiwa.

Prof. Tundui pia amesisitiza umuhimu wa kutumia AI kama nyenzo ya kujifunzia na kuongeza maarifa, badala ya kuitumia kufanya kila jambo kwa niaba ya mtumiaji.

Amesema matumizi yasiyo sahihi ya AI, hususan kwa wanafunzi, yanaweza kusababisha kupungua kwa uwezo wa kujifunza na kujenga maarifa binafsi.

“AI inaweza kumsaidia mtu kujifunza na pia inaweza kumfanya mtu kutojifunza. Ukimwambia AI kila kitu ikufanyie, unakosa maarifa,” amesema.

Kwa mujibu wa Prof. Tundui, Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kutoa elimu kwa jamii, wakiwemo vijana, kuhusu namna bora na salama ya kutumia teknolojia ya AI ili kupata manufaa yake bila kuathiri mchakato wa kujifunza na kujenga ujuzi.

Akizungumzia mradi wa DATA2INFO, Prof. Tundui amesema mradi huo umejikita katika kujenga uwezo wa wataalamu katika uchakataji na uchambuzi wa data ili kuzalisha taarifa na maarifa yatakayosaidia katika kufanya maamuzi sahihi.

Amesema data haipaswi kubaki katika mfumo wa takwimu pekee, bali inapaswa kuchakatwa na kubadilishwa kuwa taarifa na maarifa yanayoweza kutumika katika kutatua changamoto mbalimbali za jamii na kusaidia kufanya maamuzi yenye ushahidi.

“Tunatakiwa kuhakikisha data inatumika kama ushahidi, ibadilishwe kuwa taarifa na taarifa hizo kuwa maarifa ambayo yatasaidia kufanya maamuzi yenye uelewa,” amesema.

Amesema kufungwa kwa mradi huo si mwisho wa kazi, bali ni mwanzo wa kutumia mafanikio yaliyopatikana na kuyafikisha kwa wadau wengi zaidi.

Ameongeza kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kina wajibu wa kuhakikisha wataalamu waliopata ujuzi kupitia mradi huo wanakuwa mabalozi wa maarifa kwa kuwafundisha wengine namna bora ya kuchakata na kutumia data.

Kwa upande wake, Mratibu wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Alardo Barakabitze, amesema kufungwa kwa mradi huo hakupaswi kutafsiriwa kama mwisho wa ushirikiano, bali ni nafasi ya kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.

Dkt. Barakabitze amesema mradi huo umechangia kuongeza ujuzi kwa wataalamu na wahadhiri, huku baadhi yao wakipatiwa mafunzo maalum nchini Ubelgiji yaliyolenga kuimarisha uwezo wao katika kuchambua data na kuzalisha taarifa muhimu kutokana na data zilizokusanywa.

Amesema kupitia mradi huo, wataalamu wameweza pia kujengewa uwezo wa kuwasilisha matokeo ya tafiti na kutumia maarifa hayo katika kushughulikia changamoto zinazozikabili jamii.

Amewahimiza washiriki wa mradi pamoja na wataalamu wa taaluma kuhakikisha maarifa, ujuzi na nyenzo za mafunzo walizopata zinatumika ipasavyo katika kutatua changamoto za jamii.

Dkt. Barakabitze amesema ni muhimu ushirikiano huo kuendelea hata baada ya kukamilika kwa mradi, ili kuhakikisha ujuzi na mafanikio yaliyopatikana yanaendelea kuleta matokeo chanya.

“Tunapohitimisha mradi huu tusiuchukulie kama mwisho, bali tuendelee kushirikiana, kujengana uwezo na kutumia data pamoja na tafiti mbalimbali katika kutatua changamoto za jamii,” amesema.




 

0/Post a Comment/Comments