ORCI YATOA ONYO: WANAUME PIA WAPO HATARINI KUPATA SARATANI YA MATITI

.....

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dkt. Diwani Msemo, amewataka wanaume kutopuuza uvimbe unaojitokeza kwenye titi, akisisitiza kuwa wanaume pia wanaweza kuugua saratani ya matiti licha ya kuwa ugonjwa huo kuathiri zaidi wanawake.

Dkt. Msemo amesema takribani asilimia mbili ya wagonjwa wa saratani ya matiti ni wanaume, huku wanawake wakichukua sehemu kubwa ya wagonjwa hao.

Amesema matibabu ya saratani ya matiti kwa wanaume yanaweza kuhusisha tiba ya kemikali, upasuaji wa kuondoa titi pamoja na tiba ya homoni, kulingana na aina na hatua ya ugonjwa.

“Baba ukiona una uvimbe kwenye titi lako, usilichukulie kwa urahisi. Jua kabisa kwamba na wewe una nafasi ya kupata saratani ya matiti,” amesema Dkt. Msemo.

Aidha, Dkt. Msemo amesema kunyonyesha ni miongoni mwa sababu zinazoweza kusaidia kupunguza hatari ya saratani ya matiti kwa wanawake, lakini si kinga ya moja kwa moja inayomaanisha kuwa mama anayenyonyesha hawezi kupata saratani hiyo.

Ameeleza kuwa saratani ya matiti inachangiwa na mambo mbalimbali, ikiwemo vinasaba vinavyoweza kurithiwa katika familia, mazingira na aina ya vyakula, hivyo kunyonyesha ni moja tu ya mambo yanayoweza kuwa na mchango katika kupunguza hatari.

Amesema wanaume hawanyonyeshi, lakini hilo halimaanishi kuwa hawawezi kupata saratani ya matiti, kwa kuwa ugonjwa huo hautokani na suala la kunyonyesha pekee.

Dkt. Msemo ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari–Maelezo, katika mkutano wa kueleza utekelezaji wa ORCI kwa mwaka wa fedha 2025/26 pamoja na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2026/27.

Amesisitiza umuhimu wa wananchi kuwa na uelewa kuhusu saratani ya matiti na kufika hospitalini mapema wanapoona dalili zisizo za kawaida, ili uchunguzi na matibabu yaanze kwa wakati.
 

0/Post a Comment/Comments