POLISI JAMII YATOA ELIMU YA UKATILI WA KIJINSIA SHULE YA MSINGI MAZENGO

......

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Polisi Jamii mkoani Dodoma limetoa elimu kwa wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Mazengo kuhusu usalama, madhara ya ukatili wa kijinsia na namna ya kujikinga na vitendo vya uhalifu, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya Polisi Jamii nchini.

Elimu hiyo imetolewa na Kaimu Afisa Polisi Jamii Mkoa wa Dodoma, ASP Regina Mtana, wakati wa ziara ya Polisi Jamii shuleni hapo, ambapo pia walishiriki katika zoezi la usafi.

ASP Mtana amesema uchaguzi wa Shule ya Msingi Mazengo umefanyika kwa kutambua umuhimu wa shule hiyo katika jamii na mchango wake wa muda mrefu katika kutoa viongozi mbalimbali nchini.

Amesema Polisi Jamii inalenga kufanya kazi kwa karibu na wananchi kwa kuwa uhalifu unatokea ndani ya jamii na hauwezi kudhibitiwa bila ushirikiano wa wananchi na Jeshi la Polisi.

Ameeleza kuwa moja ya majukumu makubwa ya Polisi Jamii ni kuzuia uhalifu kabla haujatokea, kupitia utoaji wa elimu, kubaini viashiria vya uhalifu na kuwahamasisha wananchi kutoa taarifa kuhusu uhalifu na wahalifu.

“Tunaisogelea jamii kwa sababu jukumu letu la msingi ni kuhakikisha jamii inakuwa salama. Hatuwezi kumaliza uhalifu bila kushirikiana na raia,” amesema ASP Mtana.

Amesema wanafunzi ni sehemu muhimu ya jamii na wako katika kundi linaloweza kukumbwa na vitendo vya ukatili, hususan ukatili wa kijinsia, hivyo elimu ya kujikinga na uhalifu inapaswa kutolewa mara kwa mara mashuleni.

Ameonya wanafunzi dhidi ya kutembea katika maeneo hatarishi, hususan nyakati za usiku, akisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa au kushuhudia vitendo vya ukatili.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kikuyu Kaskazini, Heri Huseini Beji, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii, akisema hatua hiyo imechangia kupunguza uhalifu katika kata hiyo.

Amesema Polisi Jamii imekuwa ikishirikiana na jamii kupitia elimu inayotolewa na askari wa kata, jambo ambalo limewasaidia wananchi, wakiwemo watoto, kutambua hatari zinazowazunguka na namna ya kukabiliana nazo.

Diwani Begi pia ameeleza mchango wa Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Mtumba, Anthony Mavunde, ambaye alisoma katika Shule ya Msingi Mazengo, akisema amekuwa akichangia maendeleo ya shule hiyo na jamii kwa ujumla.

Amesema mchango huo umehusisha kuboresha madarasa, kujenga madarasa mapya pamoja na kusaidia huduma nyingine muhimu katika kata hiyo.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mazengo, Rehema Nkungu, amesema elimu inayotolewa na Jeshi la Polisi imekuwa na mchango mkubwa katika kubadilisha tabia za wanafunzi na kuwajengea uelewa kuhusu usalama wao.

Amesema wanafunzi wamekuwa wakitambua vitendo vya ukatili vinavyoweza kutokea nyumbani, shuleni au katika jamii na kujua maeneo sahihi ya kutoa taarifa.

“Tunashukuru sana Jeshi la Polisi kwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia kulinda usalama wa watoto kupitia elimu na Dawati la Jinsia,” amesema Rehema.

Ameongeza kuwa wanafunzi wakubwa wamekuwa mabalozi kwa kuwafundisha wanafunzi wa madarasa ya chini pamoja na familia zao kuhusu masuala ya usalama.

Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Mazengo wamesema elimu waliyopewa imewasaidia kutambua haki zao, kujua namna ya kujikinga na ukatili wa kijinsia na maeneo ya kuripoti endapo watakumbana na vitendo hivyo.

Wamesema wamejifunza madhara ya ukatili wa kijinsia, ikiwemo mimba za utotoni, maambukizi ya magonjwa ya zinaa na athari kwa maendeleo na ndoto zao, huku wakiahidi kuwafikishia elimu hiyo wanafunzi wenzao wa madarasa ya chini pamoja na familia zao.

Maadhimisho ya miaka 20 ya Polisi Jamii yanafanyika chini ya kaulimbiu inayohimiza ushirikiano wa jamii katika kudumisha amani, usalama na umoja wa kitaifa, huku elimu kwa wananchi ikitiliwa mkazo kama moja ya njia muhimu za kuzuia uhalifu.





 

0/Post a Comment/Comments