PPAA YAWANOA WAKANDARASI MAZINGIRA YA HAKI MICHAKATO YA ZABUNI ZA UMMA

*****

Na Mwandishi Wetu, Dar
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imewajengea uwezo makandarasi kuhusu mazingira ya haki katika mchakato wa zabuni za umma, ili waweze kudai haki zao pindi wanapoona hawakutendewa haki kwenye michakato ya zabuni za umma walizoshiriki.

Wasilisho la PPAA limewasilishwa na Mkuu wa Sehemu ya Huduma za Sheria PPAA, Bi. Agnes Sayi ambaye alimwakilisha Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando katika Mkutano wa Mashauriano na Wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa Mwaka 2026 ulioandaliwa na Bodi ya Wakandarasi (CRB) tarehe 13 – 14, Agosti, 2026 Jijini Dar es Salaam. 

Bi. Sayi amesema kuwa, ununuzi wa umma ni zaidi ya utaratibu wa kununua kazi za ujenzi, bidhaa au huduma; ni chombo cha sera ya maendeleo kinachochochea ukuaji wa uchumi, ajira, kuwezesha makandarasi wazawa kushiriki katika miradi ya Serikali na kuhakikisha matumizi bora ya fedha za umma. 

“Mazingira ya haki katika mchakato wa zabuni za umma ni mfumo unaohakikisha washiriki wote wanatendewa kwa usawa, wanashindana kwa kutumia masharti yanayofanana, na maamuzi yote yanafanywa kwa kuzingatia sheria, kanuni na masharti ya nyaraka za zabuni,” amesema Bi. Sayi
“Mazingira ya haki katika zabuni za umma ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” Bi. Sayi ameongeza.

Kadhalika, Bi. Sayi ameongeza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inahitaji mfumo wa ununuzi wa umma unaozingatia misingi ya haki, uwazi, uwajibikaji na ushindani wa haki. 

“Maamuzi ya PPAA yanaonesha kuwa mazingira ya haki si suala la kisheria pekee bali ni nyenzo ya maendeleo ya Taifa. Kupitia uchambuzi wa maamuzi ‘jurisprudence’ yake, PPAA imeendelea kujenga mfumo unaolinda haki za washiriki wa zabuni, unaoimarisha uwajibikaji wa taasisi nunuzi na unaoongeza imani ya sekta binafsi kushiriki miradi ya maendeleo,” ameongeza Bi. Sayi
Bi. Sayi amewasihi makandarasi, washauri elekezi, Taasisi nunuzi na wadau wengine kuzingatia sheria na kanuni za ununuzi wa umma ili kuiwezesha Serikali kuwa na mfumo wa ununuzi unaochochea ushindani, matumizi bora ya fedha za umma na utekelezaji wenye mafanikio wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Naye Bw. Steven Masangia Msanifu wa Majengo kutoka Kampuni ya Ebenezer Architects Ltd amesema kuwa makandarasi wamekuwa wakitekeleza mikataba, ila baadhi ya vipengele vya kwenye Masharti Maalum ya Mkataba yamekuwa yakiwabana na kupelekea baadhi yao kufilisika. 

“Makandarasi hawalipwi ongezeko la riba, jambo ambalo limekuwa likituathiri kiuchumi. Tunapaswa kulipwa ndani ya muda uliowekwa kwenye mkataba ili kutuwezesha kutekeleza mikataba kwa ufanisi,” amesema Bw. Masangia

Masangia ameitaka PPAA kuendelea kutoa elimu kwa wazabuni na makandarasi ili wasichanganye malalamiko/rufaa dhidi ya uamuzi wa ununuzi na migogoro inayotokana na utekelezaji wa mkataba baada ya mkataba kusainiwa.

Mkutano wa Mashauriano na Wadau wa Sekta ya Ujenzi, umewakutanisha wadau takribani 1,000 umeongozwa na Kaulimbiu, “Dira 2025: Fursaa na Wajibu wa Makandarasi katika ujenzi wa Miundombinu Endelevu”










 

0/Post a Comment/Comments