Na Carlos Claudio, Dodoma.
Pumba za mpunga ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikitupwa baada ya mavuno sasa zimeanza kugeuka kuwa fursa ya biashara kwa wajasiriamali, huku teknolojia ya kuzibadilisha kuwa mkaa mbadala ikitarajiwa kusaidia kupunguza ukataji wa miti, kuongeza ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Teknolojia na Viwanda kutoka SIDO, Mha. Kalumuna Benedicto, alipozungumza na waandishi wa habari katika warsha ya kuhitimisha mradi wa kuongeza thamani ya pumba za mpunga kwa ajili ya kuzalisha mkaa mbadala.
Mha. Kalumuna amesema pumba za mpunga ni malighafi inayopatikana kwa urahisi kwa kuwa mara nyingi hutupwa na haiuzwi kama bidhaa nyingine, hivyo kuzitumia kuzalisha nishati mbadala kunampa mjasiriamali fursa ya kupata malighafi kwa gharama nafuu.
Amesema matumizi ya teknolojia hiyo hayasaidii tu kuongeza kipato kwa wajasiriamali, bali pia yanachangia katika uhifadhi wa mazingira, uundwaji wa ajira na ukuaji wa uchumi wa taifa.
Mradi huo uliofadhiliwa na Serikali ya Japan, umeendeshwa kwa ushirikiano wa UNIDO, SIDO, Chuo Kikuu cha Nelson Mandela pamoja na kampuni ya E-Square kutoka Japan, ambapo awali kampuni tatu za wajasiriamali zilipewa mashine kupitia ufadhili huo.
Mha. Kalumuna amesema lengo kubwa la mradi huo ni kuonesha kwa vitendo kuwa mabaki ya mazao, hususan pumba za mpunga, yanaweza kuongezewa thamani na kuzalisha kuni bora au mkaa mbadala.
Amesema SIDO inalenga kuhamasisha sekta binafsi kuona fursa hiyo, wakati serikali ikiwa na wajibu wa kusaidia wawekezaji na viwanda vinavyohitaji teknolojia hiyo.
Katika hatua nyingine, SIDO imeeleza kuwa mashine ya Kijapani iliyotolewa kupitia mradi huo ina thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100, lakini uchunguzi umeonesha kuwa teknolojia hiyo inaweza kutengenezwa nchini kupitia taasisi kama SIDO, TEMDO pamoja na karakana ndogo.
Mha. Kalumuna amesema hatua hiyo itasaidia wajasiriamali ambao hawana uwezo wa kununua mashine kubwa kutoka nje ya nchi, huku wakiweza kupata mashine zinazotengenezwa ndani ya nchi kwa gharama nafuu.
Ameeleza kuwa awali mradi ulilenga viwanda, lakini uchunguzi uliofanyika umeonesha kuwa soko kubwa la mkaa huo lipo katika shule na taasisi zenye idadi ya watu zaidi ya 100, ambazo zinaweza kutumia nishati hiyo kwa ajili ya mapishi.
Kwa mujibu wake, kuni hizo za pumba za mpunga zinapatikana kwa bei ya takribani shilingi 350 hadi 500 kwa kilo, jambo linalozifanya kuwa nishati inayoweza kumudu kutumika katika taasisi na kwa wananchi wa makundi mbalimbali ya kipato.
Mratibu wa mradi wa kuongeza thamani ya pumba za mpunga kwa ajili ya kuzalisha mkaa mbadala kutoka UNIDO, Faustine Msangira, amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za kusaidia serikali kupunguza ukataji miti na kuhifadhi mazingira.
Amesema mradi huo ulitekelezwa kwa takribani mwaka mmoja na nusu katika mikoa ya Morogoro, Mbeya na Shinyanga, ambapo kampuni tatu za wajasiriamali zilipata fursa ya kupata mashine na mafunzo ya uzalishaji wa mkaa mbadala.
Ameeleza kuwa baada ya mafunzo, kampuni hizo zimeanza kuzalisha mkaa mbadala na kuweza kuajiri wafanyakazi, huku shule zikiwa miongoni mwa wateja wanaonunua bidhaa hiyo.
Faustine amesema mashine zilizotolewa ni za mfano, hivyo wajasiriamali wengine wanatakiwa kujifunza kutokana na mradi huo na kuanzisha biashara za nishati mbadala.
Mnufaika wa mradi huo na mashine, Christopher Amory Salim kutoka Raphael Group Limited, amesema teknolojia hiyo imewapa fursa ya kuzalisha na kuongeza kipato, sambamba na kuunda ajira kwa vijana na wanawake.
Amesema kupitia uzalishaji huo, vijana wamepata ajira katika uendeshaji wa mashine, wakati wanawake na vijana wengine wakipata fursa katika ukusanyaji wa pumba za mpunga.
Hata hivyo, amesema changamoto kubwa iliyopo ni soko kwa kuwa bidhaa hiyo bado ni mpya kwa watumiaji, ingawa kampuni yake imeanza kupata soko kupitia shule na taasisi.
Naye Mwenyekiti wa Motormax Energies, Ibrahim Kangamila, amesema kampuni hiyo inajihusisha na uchakataji wa mabaki ya mazao na kuyabadilisha kuwa nishati safi ya kupikia.
Amesema bado kuna haja ya kufanya maboresho zaidi katika sekta hiyo, hususan kutoa elimu kwa watumiaji kuhusu faida za nishati safi na gharama halisi za matumizi ya nishati inayotokana na miti.
Ameeleza kuwa kampuni hiyo imeanza kutoa elimu shuleni kuhusu athari za ukataji miti na umuhimu wa kutumia nishati safi, ili kuunga mkono juhudi za serikali za kulinda mazingira na afya za wananchi.






Post a Comment