Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) chenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 leo, tarehe 22 Agosti 2026, katika eneo la mradi lililopo Rufiji, mkoani Pwani.
Viongozi mbalimbali wameungana na Rais Samia katika uzinduzi huo, akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi,Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba; Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Moustafa Madbouly; Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi; pamoja na viongozi wengine.
Uzinduzi wa JNHPP ni kilele cha utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimkakati uliotekelezwa kwa kutumia fedha za ndani za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mradi huo umegharimu takribani shilingi trilioni 7.452, sawa na dola za Marekani bilioni 3.35. Ujenzi wake ulianza Juni 2019 na kukamilika Machi 2025.
JNHPP imeongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini na kuimarisha usalama wa nishati. Kwa sasa, uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini umefikia takribani megawati 4,075, ambapo JNHPP pekee inachangia zaidi ya nusu ya uwezo huo.









Post a Comment