Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewataka wafanyakazi wanaoshiriki kwenye ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Nzuguni jijini Dodoma kuhakikisha wanalinda rasilimali za taifa zinazowekezwa katika mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 300.
Senyamule ametoa wito huo jijini Dodoma wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo wa kimkakati unaojengwa mahsusi kwa ajili ya mashindano mbalimbali huku akisisitiza kila anayehusika na mradi huo ana wajibu wa kuhakikisha vifaa na miundombinu vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa
Amesema uwanja huo ni uwekezaji mkubwa wa Serikali unaolenga kuipa Tanzania, hususan Dodoma, miundombinu ya michezo yenye viwango vya kimataifa, hivyo ni muhimu kwa wafanyakazi na wataalamu wote kushirikiana kuhakikisha mradi unakamilika kwa ubora unaotakiwa.
“Macho yenu yanaona, masikio yenu yanasikia, kwa hiyo kazi yenu kubwa ni kulinda rasilimali za nchi ambazo zimewekezwa hapa.” amesema Senyamule.
Amesema Serikali imeweka fedha nyingi katika ujenzi wa uwanja huo kutokana na utashi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha Dodoma inakuwa na uwanja wenye viwango vinavyokidhi matakwa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Senyamule amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo na namna Wizara pamoja na mkandarasi, kampuni ya Limonta kutoka Italia, wanavyofuatilia utekelezaji wake, huku akieleza matumaini kuwa uwanja huo utakamilika kwa wakati ili kutoa fursa kwa timu mbalimbali kufanya maandalizi na mazoezi kuelekea AFCON 2027.
Ameongeza kuwa uwanja huo utakuwa na manufaa makubwa kwa Dodoma na Tanzania kwa ujumla, ikiwemo kuifanya Dodoma kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya michezo na kuvutia timu mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema ujenzi wa uwanja huo umefungua fursa za ajira kwa vijana, ambapo zaidi ya vijana 200 wameajiriwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo.
Amesema vijana hao wametoka katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, jambo alilolieleza kuwa ni ishara ya namna miradi mikubwa ya Serikali inavyoweza kuwa chanzo cha ajira na kuinua maisha ya wananchi.
Senyamule amewapongeza vijana hao kwa kuchangamkia fursa hiyo na kuwataka kuendelea kuwa waaminifu, huku akisisitiza kuwa vitendo vya wizi au uharibifu wa vifaa vya ujenzi vinaweza kuathiri ubora wa uwanja ambao baadaye utatumiwa na Watanzania wote.
Amesema Mkoa wa Dodoma uko tayari kushirikiana na Wizara pamoja na mkandarasi katika kutatua changamoto zitakazojitokeza ili kuhakikisha ujenzi wa uwanja huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotarajiwa.
Kwa upande wake, Mbunifu Majengo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhandisi Edwin Godfrey, ameeleza hatua ambayo ujenzi wa uwanja huo umefikia, akibainisha pia uwezo wa uwanja huo ambao unatarajiwa kuwa na nafasi ya kuchukua idadi kubwa ya watazamaji.



Post a Comment