RIDHIWANI KIKWETE ATEMBELEA BANDA LA WHI KATIKA MAONESHO YA NANENANE DODOMA

 

******

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, ametembelea banda la Watumishi Housing Investments (WHI) katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma.

Mhe. Kikwete alipokelewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa WHI, Bw. Sephania Solomon, ambaye alimweleza kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo. Miongoni mwa huduma hizo ni uwekezaji kupitia Faida Fund, mfuko wa uwekezaji unaotoa faida ya zaidi ya asilimia 13 kwa mwaka, fursa za ununuzi wa nyumba za gharama nafuu katika maeneo mbalimbali nchini, pamoja na huduma za nyumba za kupanga.

Mhe. Kikwete alipongeza WHI kwa juhudi zake za kuwafikia wananchi na kutoa huduma zinazochangia kuwawezesha Watanzania kumiliki nyumba na kuwekeza kwa urahisi.

Aidha, WHI ni Mkandarasi wa Daraja la Kwanza na imehusika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi nchini, ikiwa kama mshauri elekezi (consultant) au mkandarasi (contractor). Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa jengo la ofisi za UCSAF jijini Dodoma na jengo la Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, pamoja na miradi mingine mingi. Wananchi wanaotembelea banda la WHI wanapata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu miradi hiyo na huduma nyingine zinazotolewa na taasisi ya WHI.

WHI inawakaribisha wananchi wote kutembelea banda lake lililopo katika Banda Kuu la Ofisi ya Rais, Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye Maonesho ya Nanenane jijini Dodoma, ili kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji, umiliki wa nyumba na huduma nyingine zinazotolewa na taasisi ya WHI.












0/Post a Comment/Comments