********
Na. OWM (KAM), Lindi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amewataka viongozi wa mikoa ya Kanda ya Kusini kutumia Maonesho ya Nane Nane kuhamasisha jamii kula na kutumia bidhaa za korosho ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Waziri Sangu ametoa wito huo leo, Jumanne Agosti 5, 2026, katika Viwanja vya Ngongo, Wilaya ya Lindi, alipokuwa mgeni rasmi katika Siku Maalum ya Ulaji wa Korosho. Siku hiyo ni sehemu ya Maonesho ya Nane Nane ya Kanda ya Kusini yanayoshirikisha mikoa ya Lindi na Mtwara.
"Kanda ya Kusini mmejipanga vizuri kutekeleza Dira 2050 kupitia Maonesho ya Nane Nane. Wakulima na wajasiriamali mmeuratibu vizuri kupata elimu, ikiwemo fursa za kuongeza mitaji kupitia taasisi za fedha," alisema Sangu.
Akizungumzia zao la korosho na mnyororo wa thamani, Waziri Sangu alisema jitihada zaidi zinatakiwa ili mchango wa zao hilo katika ukuaji wa uchumi uongezeke.
Alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wakulima wa korosho wanapata masoko ya uhakika na bei nzuri.
"Tunatakiwa tuendelee kuongeza thamani ya korosho yetu badala ya kuiuza mbichi. Hii itasaidia vijana kupata ajira na kodi kwa serikali kuongezeka," aliongeza.
Akiwa kwenye banda la Halmashauri ya Mtwara ,Waziri Sangu alikagua shughuli za wajasiliamali na kuwapongeza kwa kuongeza thamani mazao ya biashara ikiwemo korosho.
Katika kutambua umuhimu wa wajasiliamali, Waziri Sangu amewafahamisha uwepo wa soko la Afrika Mashariki kupitia maonesho ya Juakali ambapo serikali itagharamia wajasiliamali 250 kwenda kushiriki nchini Rwanda.
Kufuatia hatua hiyo Waziri Sangu alielekeza uongozi wa mikoa ya kanda ya kusini kuratibu upatikanaji wa wajasiliamali watakaokwenda kushiriki kwenye maonesho ya wajasiliamali wadogo na wa kati ya Afrika Mashariki maarufu kama Juakali yatakayofanyika Kigali nchini Rwanda Oktoba 30 mwaka huu.
Kwa upande wake, Mratibu wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kusini, Mwinyijuma Mkungu, alisema jumla ya wadau 160 kutoka halmashauri 15 za mikoa ya Lindi na Mtwara wanashiriki maonesho hayo.
Mkungu alibainisha kuwa lengo la kuadhimisha Siku Maalum ya Ulaji wa Korosho ni kuhamasisha Watanzania kula korosho na kutumia bidhaa zake mbalimbali.
Alisema kupitia ulaji na matumizi ya korosho, thamani ya zao hilo itaongezeka na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa Kanda ya Kusini.
Aidha, alieleza kuwa maonesho hayo pia ni jukwaa la kuwapa wakulima na wajasiriamali fursa ya kujifunza teknolojia mpya za uzalishaji na uongezaji thamani wa korosho.
Waziri Sangu alipata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali ya wadau walioshiriki maonesho hayo na kuzungumza na wakulima na wafanyabiashara.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea ambaye pia ni Kaimu Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mohamed Moyo alisema maonesho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 inayolenga kuwezesha wakulima na wavuvi kupata elimu itakayosaidia kuchochea mabadiliko chanya ya kiuchumi.
Waziri Sangu anaendelea na ziara yake mkoani Lindi kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.
MWISHO









Post a Comment