SUA YAWEKA MFUMO WA “PENSENI” KWA PANYA WASTAAFU, MAGAWA AWEKA HISTORIA CAMBODIA

......

Na Carlos Claudio, Dodoma

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Raphael Chibunda, amesema chuo hicho kimeweka mfumo maalumu wa kuwahudumia panya wanaotumika katika tafiti na mafunzo ya kisayansi, ikiwamo kuwapatia huduma baada ya kustaafu.

Profesa Chibunda amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za SUA kwa mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka unaofuata, katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mtumba.

Amesema mradi wa ufugaji, mafunzo na utafiti wa panya katika SUA umedumu kwa zaidi ya miaka 25, huku panya hao wakiwa na asili ya Tanzania, hususan kutoka Milima ya Uluguru mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa Profesa Chibunda, SUA kwa sasa ina kituo maalumu kinachohusika na uzalishaji, malezi na mafunzo ya panya hao kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya tafiti na shughuli za kisayansi.

Ameeleza kuwa chuo hicho kimeweka mfumo unaozingatia hatua mbalimbali za maisha ya panya hao, kuanzia wanapozaliwa, wanapokuwa katika mafunzo, wanapohitimu na hatimaye wanapostaafu.

“Ukimfika kwetu utakuta tuna wodi ya wazazi, tuna wanaoanza mafunzo, waliohitimu, lakini pia tuna banda la panya wastaafu... wako pale wanapata pensheni,” amesema Profesa Chibunda.

Akizungumzia historia ya panya maarufu duniani Magawa, Profesa Chibunda amesema panya huyo alikuwa miongoni mwa panya waliopatiwa mafunzo nchini Tanzania na baadaye kupelekwa Cambodia kwa ajili ya kusaidia kutambua mabomu ya ardhini.

Amesema Magawa aliweka historia kubwa baada ya kufanikiwa kugundua mabomu mengi ya ardhini, hatua iliyomfanya kutambulika kimataifa na kutunukiwa medali ya heshima kutokana na mchango wake.

Profesa Chibunda amesema Tanzania haikuwa na mazingira yenye changamoto kubwa ya mabomu ya ardhini kama ilivyokuwa Cambodia, hivyo panya hao walitumwa kwenda kusaidia katika eneo hilo.

Ameeleza kuwa panya hao wana wastani wa maisha wa takribani miaka minane, na wanapofikisha umri wa miaka tisa huwa katika hatua ya uzee mkubwa, ambapo baadhi yao huanza kupoteza meno na uwezo wao wa kufanya kazi hupungua.

Kwa mujibu wa Profesa Chibunda, Magawa aliishi hadi kufikia hatua hiyo ya uzee akiwa Cambodia, ambako hatimaye alifariki dunia.

Akizungumzia uwezekano wa Magawa kurejeshwa Tanzania baada ya kifo chake, Profesa Chibunda amesema mpango huo uliwahi kuwepo, lakini haukuweza kutekelezwa kutokana na changamoto za taratibu na vibali vya usafirishaji.

“Tunasema ingewezekana, lakini kwa wakati ule taratibu na vibali vya kilojistiki viligoma. Wenzetu kule Cambodia walikosa uvumilivu wa kusubiri, wakamjengea mnara mkubwa kule,” amesema.

Amesema SUA inaendelea kutumia panya hao katika tafiti na mafunzo ya kisayansi, huku ikizingatia ustawi wao katika hatua zote za maisha, ikiwamo kipindi cha baada ya kustaafu.


 

0/Post a Comment/Comments