Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani zimekubaliana kuendelea na kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za kimkakati, ikiwemo biashara na uwekezaji, afya, mazingira, maji, uchumi wa buluu, ujenzi wa miundombinu, teknolojia na utawala bora, kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Hayo yamejili leo, Agosti 13, 2026, jijini Dodoma wakati wa mazungumzo kati ya viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na ujumbe kutoka Ujerumani. Kwa upande wa Tanzania yameongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, na Katibu Mkuu Balozi Dkt. Samwel Shelukindo huku kwa upande wa Ujerumani yakiongozwa na Mkuu wa Kitengo kinachoshughulikia masuala ya Afrika katika Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo Mhe. Joachim Schmitt.
Akizungumza na ujumbe huo, Waziri Dkt. Kombo na Katibu Mkuu Balozi Dkt. Shelukindo wamepongeza mchango wa Ujerumani katika shughuli mbalimbali za maendeleo nchini Tanzania, huku wakisisitiza utayari wa Serikali ya Tanzania kuendelea kushirikiana na Ujerumani katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii ili kuboresha ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake, Mhe. Schmitt amesema Ujerumani inaendelea kuiona Tanzania kuwa mshirika muhimu wa maendeleo barani Afrika na imedhamiria kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Ameeleza kuwa Serikali ya Ujerumani iko tayari kutazama maeneo mapya ya ushirikiano yanayoendana na mahitaji na fursa zilizopo, ikiwemo teknolojia, ulinzi na usalama pamoja na uchumi wa kidijitali.
Ujerumani ni miongoni mwa nchi kumi zinazoongoza kwa uwekezaji wa kigeni nchini Tanzania. Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), kufikia Oktoba 2025, miradi 187 ya uwekezaji kutoka Ujerumani ilikuwa imesajiliwa nchini, ikiwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 535.63 na kutoa fursa za ajira taktribani 16,427 katika sekta mbalimbali za uchumi.
Ushirikiano huo unaakisi uhusiano wa muda mrefu na unaoendelea kukua kati ya Tanzania na Ujerumani, huku pande zote zikilenga kuutumia kama msingi wa kukuza biashara na uwekezaji, kuhamasisha maendeleo endelevu na kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.













Post a Comment