......
Na Ester Maile Tanga
SERIKALI imesema inaendelea kuwaandaa vijana wa Kitanzania wenye ujuzi na vipaji mbalimbali ili kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya ujuzi ya Afrika na baadaye dunia kupitia mfumo wa WorldSkills, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha elimu inayozingatia ujuzi na mahitaji ya soko la ajira.
Akizungumza leo Agosti 20, 2026 wakati wa Wiki ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu jijini Tanga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema Serikali inatumia mbinu mbalimbali kuwajengea wanafunzi ujuzi wa vitendo, ikiwamo kuwatoa darasani na kuwapeleka katika mazingira halisi ya kazi pamoja na kuwashirikisha katika mashindano ya ujuzi yanayoratibiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTVET).
Prof. Nombo amesema Tanzania, baada ya kuwa mwanachama wa mfumo wa WorldSkills, imeanza kuweka mazingira ya kuibua na kukuza vijana wenye vipaji na ujuzi kuanzia mashindano ya ngazi za chini hadi kufikia majukwaa ya kimataifa.
Amesema vijana wanaoshiriki mashindano hayo ni miongoni mwa waliothibitisha uwezo katika fani zao na wanaendelea kutathminiwa ili kubaini watakaoiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Afrika na baadaye dunia.
Amesema maandalizi ya vijana hao yanahitaji ushirikiano wa Serikali, taasisi za elimu, wataalamu na sekta binafsi, kwa kuwa hakuna upande mmoja unaoweza kufanikisha lengo hilo.
Prof. Nombo amesema wataalamu kutoka taasisi mbalimbali, zikiwamo taasisi za mafunzo ya ufundi na utalii, wamekuwa wakishiriki kuwaandaa vijana kwa kuzingatia viwango vinavyotumika katika mashindano ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Prof. Nombo, wataalamu kutoka Tanzania pia wanapata uzoefu kuhusu namna mashindano ya kimataifa yanavyoendeshwa, mifumo ya tathmini na maandalizi ya washiriki.
Amesema baadhi ya wataalamu tayari wamepata mafunzo kutoka kwa wadau wa mashindano ya ujuzi ya kimataifa, hivyo mashindano yanayoendelea nchini yanaandaliwa kwa kuzingatia vigezo vya kimataifa.
Katika hatua nyingine, Prof. Nombo amesema Serikali inaendelea kusimamia elimu jumuishi kwa kuhakikisha vijana wenye mahitaji maalum wanapata fursa ya kuonyesha vipaji na uwezo wao.
Amesema ushiriki wao katika mashindano hayo unaonyesha kuwa changamoto za ulemavu si kikwazo cha kutumia kipaji na kuchangia maendeleo ya taifa, huku Serikali ikilenga kujenga kundi la vijana wenye ujuzi wa hali ya juu watakaoweza kushindana na wenzao Afrika na duniani.

Post a Comment