TRA YAWEKA KAMBI KIZIMKAZI FESTIVAL HUDUMA ZA KODI ZAENDELEA KUTOLEWA

*****
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeweka kambi ya huduma kwenye banda lake la maonyesho katika Tamasha la Kizimkazi na maonyesho ya biashara ambako huduma mbalimbali za kikodi zinaendelea kutolewa kwa wananchi wanaotembelea banda hilo.

Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda ametembelea banda hilo la huduma la TRA Agosti 13, 2026 na kutoa Vyeti vya namba za utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa baadhi ya wananchi waliotembelea banda hilo akisisitiza kuwa Wafanyabiashara wanaopatiwa TIN mpya watakapa msamaha wa kodi kwa muda wa mwaka mmoja.

Amesema utaratibu huo unalenga kusajili walipakodi wengi zaidi ili kuongeza wigo wa kodi na kukuza biashara nchini hali ambayo itasaidia kuchochea shughuli za uchumi kwa wananchi. 

Amesema katika utendaji kazi wake TRA imekuwa ikiwafuata wananchi katika maeneo yao ya biashara kuwasikiliza, kutatua changamoto zao na kuwezesha biashara zao.

Kamishna Mkuu Mwenda ametoa wito kwa Walipakodi kutembelea maonyesho ya biashara kwenye Kizimkazi Festival ili kupata huduma za TRA zinazoendelea kutolewa.

Kwa upande wake mmoja wa wananchi waliopatiwa TIN Bw. Yusuph Mabrook Juma ameishukuru TRA kwa kuwasogezea huduma karibu na maeneo yao na kuwapatia elimu ya kodi itakayowawezesha kutambua umuhimu wa kulipa kodi.

Amesema katika banda la TRA pia amepatiwa elimu ya namna ya kuendesha biashara zake hali ambayo itamsaidia kuinuka kiuchumi. 






 

0/Post a Comment/Comments