TUME YA MADINI YATOA SIKU 30 KWA MIRADI YA UCHIMBAJI MDOGO KUREKEBISHA MAPUNGUFU

......

Na Carlos Claudio, Dodoma

Tume ya madini imewapa muda wa siku 30 wamiliki na wawezeshaji wa miradi ya ucimbaji mdogo inayotekelezwa kupitia mikataba ya msaada wa kiufundi, kurekebisha mapungufu yaliyobainika katika ukaguzi, la sivyo watakabuliwa na hatua za kusheria

Hatua hiyo imekuja baada ya Tume ya Madini kufanya ukaguzi katika miradi 128 ya uchimbaji mdogo, ambapo miradi 42 ilibainika kuwa haifanyi kazi, huku miradi mingine 86 ikiendelea na shughuli za uchimbaji lakini ikiwa na mapungufu katika utekelezaji wa shughuli zake na uzingatiaji wa masharti ya Mikataba ya Msaada wa Kiufundi.

Akizungumza jijini Dodoma, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, amesema wamiliki wa miradi 42 iliyobainika kutofanya kazi wamepewa Hati za Makosa zenye muda wa siku 30, ili kutoa mrejesho wa hatua walizochukua kurejesha shughuli za uchimbaji kwa mujibu wa sheria na masharti ya ridhaa za Msaada wa Kiufundi.

Mhandisi Lwamo amesema ukaguzi huo ulifanyika kufuatia maelekezo ya Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, yaliyotolewa Aprili 27, 2026, wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema katika miradi 86 inayoendelea na shughuli za uchimbaji, Tume ilibaini changamoto mbalimbali, ikiwemo kutotekelezwa ipasavyo kwa mipango inayotakiwa kisheria.

Mipango hiyo ni pamoja na Mpango wa Usimamizi wa Mazingira, Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), Mpango wa Uhawilishaji wa Teknolojia, Mpango wa Uchimbaji pamoja na Mpango wa Ufunguaji wa Mgodi.

Kwa mujibu wa Mhandisi Lwamo, wamiliki wa miradi hiyo pamoja na wawezeshaji wa Msaada wa Kiufundi wanapaswa kurekebisha mapungufu hayo ndani ya siku 30, kwa kuzingatia Kanuni za Msaada wa Kiufundi kwa Wamiliki wa Leseni Ndogo za Uchimbaji Madini za mwaka 2025.

Ameonya kuwa endapo wahusika watashindwa kutekeleza matakwa hayo ndani ya muda uliowekwa, Tume ya Madini itachukua hatua zaidi za kisheria, ikiwemo kufuta ridhaa za Msaada wa Kiufundi.

Wakati huo huo, Tume ya Madini imesema itaendelea kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara katika miradi inayotekelezwa kupitia Msaada wa Kiufundi, kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa kuzingatia Sheria ya Madini, kanuni zake na masharti ya ridhaa zilizotolewa.

Aidha, Mhandisi Lwamo amewataka wanufaika wa Msaada wa Kiufundi pamoja na wachimbaji wadogo kuzingatia kwa ukamilifu masuala ya usalama, afya mahali pa kazi na utunzaji wa mazingira.

Amesisitiza pia umuhimu wa wachimbaji kuchukua tahadhari zaidi wakati wa shughuli za uchimbaji, hususan katika kipindi hiki cha tahadhari kuhusu uwezekano wa mvua za El Niño, ili kuepusha madhara kwa wachimbaji, mali na mazingira yanayozunguka maeneo ya migodi.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Tume ya Madini kuimarisha usimamizi wa uchimbaji mdogo nchini, kuhakikisha Msaada wa Kiufundi unatolewa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa, huku ukichochea tija, usalama na uendelevu wa shughuli za uchimbaji madini.


 

0/Post a Comment/Comments